Mzee
wa mila ambaye pia ni kiongozi wa kikundi cha ngoma cha Kasanga kutoka
Tukuyu Wilayani Rungwe akiwa ameshikilia kombe na fedha taslimu shilingi
Milion Moja baada ya kuibuka washindi wa kwanza wakicheza ngoma yao
aina ya Ling'oma.
WANANCHI wameaswa kupenda utamaduni wa Asili
hususani ngoma za Makabila ili kuenzi mila na desturi zilizoachwa na
mababu tangu zamani na siyo kuegemea katika nyimbo za kizazi kipya.
Mwito huo ume na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa
Mbeya, Leonard Magacha wakati akifungua mashindano ya Ngoma za Asili
yaliyofanyika katika Viwanja vya Chuo cha Uhasibu(TIA) Jijini hapa.
Magacha amesema mashindano ya ngoma za asili
yatasaidia kuamsha ari ya kupenda utamaduni wa Mtanzania kwa kuenzi Mila na
Desturi zilizoachwa na waliotanguliatangu zamani kabla ya sayansi na teknolojia
ambapo vifaa vya asili vilitumika.
Ameongeza kuwa kupitia mashindano hayo itakuwa
chachu ya kufufua utamaduni vijijini ikiwa ni pamoja na kupima utendaji kazi wa
Maafisa utamaduni wa Wilaya kwa kuhamasisha na kuwafundisha wananchi kuzipenda
ngoma za asili.
Kwa upande wake Afisa Michezo na Utamaduni wa
Mkoa wa Mbeya, George Mbigima, amesema kama Mkoa utandaa mashindano makubwa
mwakani ambayo yataanzia kwenye ngazi ya Kijiji, kata, Wilaya na hatimaye
kumpata mshindi wa Mkoa.
Naye Mkuu wa Matukio wa kampuni ya Bia Tanzania
(TBL) kanda ya Mbeya, Geophrey Mwangungulu ambao ndiyo waandaaji wa Mashindano
hayo amesema lengo la kuandaa tukio hilo ni kuhamasisha wananchi kupenda ngoma
za asili pamoja na utamaduni.
Amesema jumla ya vikundi 26 vilijitokeza
kushiriki mashindano hayo kutoka katika Wilaya za Mbeya, Rungwe, Kyela,Mbozi
Njombe na Iringa ambapo katika Mashindano hayo Mshindi wa Kwanza aliibuka na
kitita cha fedha taslimu Milion moja na Kikombe.
Mshindi wa pili aliibuka na shilingi laki tano
huku mshindi wa Tatu akiondoka na shilingi laki mbili na washiriki wengine
wakiambulia kifuta jasho cha shilingi 50,000/= kwa kila kundi.
Katika mashindano hayo yaliyokuwa kivutio kwa
mamia ya Wakazi wa Mbeya kikundi cha ngoma cha Kasanga maarufu kwa Ing’oma
kutoka Wilayani Rungwe ndiyo walioibuka kidedea katika kinyang’anyiro hicho.
Nafasi ya pili ilienda kwa kikundi cha ngoma za
asili cha Lipango kutoka Isansa Wilayani Mbozi na Nafasi ya Tatu ikinyakuliwa
na Kikundi cha Mbeta kutoka Isyesye Jijini Mbeya.
Na Mbeya yetu
Post a Comment