Tanzania Football Federation
FIFA
KUCHUNGUZA KWA KINA MCHAKATO WA UCHAGUZI TFF
OFISA Maendeleo wa Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) Kusini mwa Afrika, Ashford Mamelodi
amewahakikishia Watanzania kuwa ujumbe wa Shirikisho hilo utakaokuja nchini mwezi
ujao, utafanya uchunguzi wa kina kuhusu mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (FIFA) na kutoa uamuzi kwa maslahi ya
mchezo huo.
“Ninafurahi kwamba hali ya utulivu imefikia kiwango hiki na nina
uhakika FIFA itafanya uchunguzi wa kina na kufanya uamuzi kwa maslahi ya mpira
wa miguu,” amesema Mamelodi alipokuwa akizungumzia uchaguzi mkuu wa TFF ambao
ulikuwa ufanyike Februari 24 mwaka huu lakini ukasimamishwa kutokana na
matatizo kadhaa baada ya baadhi ya wagombea kuenguliwa.
Mbali na kuhudhuria Mkutano Mkuu wa TFF na uchaguzi, safari ya
Mamelodi nchini pia ilihusisha kumtambulisha msaidizi wake, Patrick Onyango
ambaye amejiunga na ofisi hiyo ya FIFA kuanzia mwishoni mwa mwaka jana, kufuatilia
miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na GOAL Project 4 ambayo ni uwekaji wa
nyasi bandia kwenye Uwanja wa Nyamagana na maendeleo ya Uwanja wa Gombani
kisiwani Pemba, mikakati ya mwaka 2013 na kozi mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Mikutano wa
TFF jana, Mamelodi alisema uamuzi wa Shirikisho hilo kutuma wajumbe katikati ya
mwezi ujao unatokana na mawasiliano baina ya Rais wa TFF, Leodegar Tenga na
FIFA ambayo ilitaarifiwa hali halisi ilivyo na kama inaweza kusaidia kutatua
matatizo yaliyopo.
“FIFA haitakuja kuingilia mchakato wa uchaguzi, itakuja kutatua
matatizo,” amesema Mamelodi. “Masuala ya uchaguzi ni ya ndani ya nchi. FIFA
haiji kuichagulia Tanzania rais. Wajumbe wanaweza kumchagua mtu yeyote wanayeona
kuwa anafaa kuwa rais,” amesema Mamelodi.
“Lakini katiba ya FIFA iko wazi kwamba mwanachama wake ni lazima
akubaliane na sheria za Shirikisho kuwa wanachama ni lazima wabanwe na Katiba
ya FIFA. Kwa hiyo mara tu unapopata uanachama wa FIFA, ni lazima ujue kuwa utabanwa
na katiba ya FIFA na mojawapo ya mambo haya.
“Lakini kuna tofauti na kitendo cha Serikali kusimamisha uchaguzi
kwa kuwa hiyo inakuwa ni Serikali kuingilia moja kwa moja masuala ya mpira wa
miguu, kitu ambacho katiba ya FIFA inakataza.”
Mamelodi, ambaye alitumia muda mwingi kuelezea umuhimu wa hali ya
utulivu iliyotawala kwa muda mrefu nchini, amesema anajua kuwa uongozi wa Rais
wa sasa wa TFF, Leodegar Tenga umefanya mengi katika kuhakikisha unajenga
mazingira mazuri ya maendeleo ya mpira wa miguu, lakini kuna wakati ni lazima
uheshimu uamuzi wa mtu.
“Tenga amesema imetosha anaondoka na hatuna budi kuheshimu uamuzi
wake. Hiyo ni kauli inayotoka kwa kiongozi wa kweli, kiongozi anayewajibika.
Lakini kwa kuangalia misingi ambayo uongozi wake umeijenga, ni wazi kuwa
kiongozi mpya ataendeleza taasisi bila ya matatizo.
“Tanzania haikufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika, lakini
kuna miradi mingi ya maendeleo ambayo ilifanyika, mingine ambayo ilijaribiwa
kwa mara ya kwanza nchini Tanzania na ikafanikiwa. Kuna Azimio la Bagamoyo, Semina
ya Mawasiliano ya Jamii (Comm-Unity) ya Wanawake, Futuro III na mingine. Yote
hii ilifanyika kwa sababu kulikuwa na utulivu.
“Hivi sasa TFF ina sekretarieti ina Mkurugenzi wa Ufundi; ina
programu za maendeleo na kuna utulivu. Cha msingi ni kuendeleza haya. Kama
mambo haya yataendelezwa baada ya uchaguzi, ni dhahiri kuwa mpira utazidi
kuendelea. Hakuna njia ya mkato katika maendeleo.”
Uchaguzi wa TFF ulihusisha nafasi za rais, makamu wa rais na
wajumbe wa Kamati ya Utendaji kutoka Kanda 13 za Shirikisho.
Post a Comment