RAIS WA TFF TENGA ASEMA HANA MPANGO WA KUGOMBEA UONGOZI TFF
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
Leodegar Tenga amesema hatagombea tena wadhifa huo katika uchaguzi uliopangwa
kufanyika Februari 24 mwaka huu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye ofisi za TFF
leo, Rais Tenga amesema wakati anaingia kwenye uongozi mwaka 2004 ajenda ilikuwa
na kuijenga TFF kama taasisi kwa kuweka mifumo ya uendeshaji ikiwemo kutengeneza
katiba na kanuni, jambo ambalo limefanyika.
“Wajumbe wamekuwa wakiniuliza Rais vipi? Mimi hapana.
Nilishafika pale pa kufika. Tulipoanza wakati ule ilikuwa ni kujenga taasisi. Na
kazi hiyo tumeifanya. Tulipoingia mwaka 2004 hiyo ndiyo ilikuwa ajenda,” amesema
Rais Tenga.
Amesema walitengeneza Katiba, vyombo huru vya kufanya
uamuzi, kuongeza wigo wa wapiga kura ambapo hivi sasa kwenye mpira wa miguu
hakuwezi kutokea migogoro, hata ikitokea kuna mfumo wa
kuidhibiti.
Rais Tenga ameishukuru Sekretarieti ya TFF, Kamati ya
Uchaguzi ya TFF, kamati za uchaguzi za wanachama wa TFF na vyama wanachama wa
TFF kwa hatua iliyofikiwa katika uchaguzi ambapo mikoa yote imekamilisha
uchaguzi na kubaki vyama shiriki pekee.
Ametoa mwito kwa wadau kujitokeza kugombea uongozi TFF,
kwani baada ya kujenga taasisi ajenda iliyobaki ni mpira wa miguu wenyewe
ikiwemo nini kifanyika ili mpira uchezwe katika maeneo
mbalimbali.
“Tumeshatengeza mfumo, sasa ni kuangalia jinsi ya
kuendeleza mpira. Changamoto ni tufanye nini ili mpira uendelee. Tunataka watu
wengine wabebe hiyo ajenda ili tuangalie tunakwendaje mbele,”
amesema.
Pia amesema ushirikiano ambao amepata kwa wapenzi na
wadau wa mpira wa miguu ni wa ajabu. Vilevile ameishukuru vyombo vya habari,
Serikali, klabu, wadhamini na wafadhili kwa mchango wao katika uendeshaji wa
mpira wa miguu nchini.
19 WACHUKUA FOMU UCHAGUZI TFF
Wadau 19 wamechukua fomu kuwania nafasi mbalimbali za
uongozi katika uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
unaotarajiwa kufanyika Februari 24 mwaka huu.
Fomu hizo zimeanza kutolewa leo (Januari 14 mwaka huu)
ambapo wawili wamechukua nafasi ya Makamu wa Rais wakati waliobaki wanaomba
ujumbe wa Kamati ya Utendaji wakiwakilisha kanda mbalimbali.
Waliochukua fomu za umakamu wa rais ni Wallace Karia na
Ramadhan Nassib. Wote ni wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF inayomaliza muda
wake.
Waliochukua fomu za ujumbe ni Shaffih Dauda, Athuman
Kambi, Hussein Mwamba, Stewart Masima, Yusuph Kitumbo, Mugisha Galibona,
Vedastus Lufano, Twahili Njoki, Charles Mugondo, Elley Mbise, Farid Nahdi, Ayubu
Nyaulingo, Nazarius Kilungeja, Epaphra Swai, Khalid Abdallah, James Mhagama na
Selemani Bandiho.
PONGEZI UONGOZI MPYA KATAVI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa
pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Katavi (KAREFA)
uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika jana (Januari 13 mwaka
huu).
Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama
hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa KAREFA walivyo na imani kubwa
kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Katavi.
TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya
Utendaji ya KAREFA chini ya ukatibu wa Peter Hella aliyeibuka mshindi katika
uchaguzi huo uliofanyika ukumbi wa DC mjini Mpanda kwa kumshinda Emmanuel Chaula
kwa kura sita dhidi ya mbili.
Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni
kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Katavi kwa kuzingatia
katiba ya KAREFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu
yake.
Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya KAREFA na
Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa
Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Viongozi waliochaguliwa ni Hella (Katibu), Elias Mande
(Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF) na Deo Bakuba (Mwakilishi wa Klabu TFF). Nafasi ya
Mwenyekiti haikuwa na mgombea wakati Mawazo Maso aliyekuwa mgombea pekee wa
nafasi ya Makamu Mwenyekiti alipata kura nyingi za hapana. Nafasi zilizo wazi
zitajazwa katika uchaguzi mdogo.
Post a Comment