ZNZ
Yanga wanavyoipa Simba ubingwa
NA JIMMY CHIKA
MAPEMA katikati ya mwezi huu, mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara unatarajiwa kuanza kutimua vumbi nchini kote, ikiwa ni hatua ya mwisho kuelekea kumpata bingwa wa soka nchini msimu huu.
Timu za Simba na Yanga ndiyo zinazopishana kileleni, huku wana-Msimbazi wakiwa juu kwa kujikusanyia pointi 27, wakati watani wao wa jadi, wana-Jangwani, wakiwa wamemaliza mzunguko wa kwanza wakiwa na pointi 25.
Katika matukio yaliyojiri kwa mwezi mzima uliopita, Yanga wamesikika zaidi wakikabiliwa na migogoro ya ndani kwa ndani, huku Simba wakitangaza kujipanga zaidi na kuongeza nguvu katika safu yake ya ushambuliaji.
"Wanachana wapeleka nyaraka serikalini kuukataa uongozi wa Mwenyekiti Lloyd Nchunga, nyota mwingine wa timu hiyo, Jerry Tegete kutimkia Azam, mdhamini mkuu wa timu hiyo, Yusuf Manji atofautiana na Makamu Mwenyekiti Davis Mosha, Yanga yazuiwa kufanya usajili mpaka ilipe milioni 7.5, kiungo wa Yanga Athumani Idd ‘Chuji’ atofautiana na mengine kadha wa kadha."
Hizo ndizo habari angalau kwa uchache zilizopamba vichwa vya habari katika vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini. Hii ni kusema Yanga haisomi alama za nyakati?
Kwa historia, migogoro ndiyo inayozorotesha timu hizi kubwa za Yanga na Simba kwa asilimia 100 na siyo soka la uwanjani.
Mara nyingi Simba au Yanga zinapoguswa na migogoro ya uongozi, basi matokeo yanayofuata ni timu hizo kufanya vibaya uwanjani.
Hiyo inatokana na ukweli kwamba sababu inayotumiwa na aina ya viongozi wa klabu hizi ni kuhujumu timu pale wanapohisi kutotendewa haki.
Kwao, Yanga wanafahamu kwamba ligi inapoanza tu, wanaanza na deni la pointi mbili ili wafikie idadi ya pointi za watani wao Simba, ili ijiweke vizuri katika harakati za kuwania ubingwa, watatakiwa waanze kukimbia na siyo kutembea.
Lakini la ajabu, kinachotajwa kufanyika kwenye klabu hiyo kongwe nchini kwa sasa wakijiandaa na michuano hiyo ni kutimua uongozi, au wachezaji kutimka.
Baya zaidi, ni migogoro inayopenya hadi kwenye benchi la ufundi na kuzua taarifa za kocha kukwaruzana na wachezaji. Hivi jibu la matokeo ya haya yote ni nini?
Tukirudi nyuma kidogo ilivyokuwa kwenye miaka 1992 wakati huo klabu ya Yanga ikiwa chini ya mfadhili Abbas Gullamali, ilitokea wakati mfupi sana alijitoa kwa madai ya kutoelewana na uongozi.
Walichofanya viongozi wa wakati huo, walirudi vitini na kuketi wakarejesha umoja baada ya kukumbushana lengo halisi la kuundwa kwa klabu hiyo na kukuta kwamba malengo yao ya kuimarisha timu ya soka, na baina ya wana-Yanga kuwa kitu kimoja na kusaidiana katika dhiki na faraja, yamekiukwa.
Walipomaliza kikao hicho, aliyekuwa katibu shupavu wakati huo, George Mpondela, alitangaza kurudi kwa mshikamano baina ya wana-Yanga wote kuanzia viongozi, wafadhili, wachezaji hadi mashabiki.
Matunda ya maazimio hayo ilikuwa kama ifuatavyo:-
Aprili 12, mwaka 1992 timu ya Yanga ilikuwa ikikabiliwa na kibarua kigumu katika Ligi ya Tanzania Bara enzi hizo.
Ilikuwa ni siku ya mechi muhimu dhidi ya Simba ambao wakati huo ilikuwa imejiimarisha na washabiki wake kutangaza takriban kila kona ya nchi kwamba ingeiadhiri Yanga kwa idadi kubwa ya mabao.
Matokeo yake, Yanga ilishinda mchezo huo kwa kuifunga Simba bao 1-0, bao hilo likifungwa na mchezaji wa nafasi ya ulinzi wa kushoto, Kenneth Mkapa katika dakika ya 10.
Sifa ya ushindi katika mchezo ule ilielekezwa zaidi kwa viongozi ambao baadaye walifanya tafrija ya kupongezana, huku wakirudia kupaza sauti ya kutaka mshikamano baina yao uongezeke.
Kwa kumbukumbu nzuri, mechi hiyo ilikuwa na mvutano kwa vile ilipaswa kuchezwa Jumamosi badala ya Jumapili kutokana na maombi ya Yanga waliokuwa wakirejea nchini kutoka nchini Misri.
Kuhusu athari ndani ya vilabu vya soka nchini kati Simba na Yanga, inayonyesha kwamba Yanga ndiyo iliyowahi kupata athari zaidi za mpasuko.
Mwaka 1975, Yanga ilikumbana na mgogoro uliosababisha wachezaji wengi na viongozi kutimka na kwenda kuanzisha klabu ya Pan.
Kutokana na mgawanyiko huo, Yanga ilipata kipigo kikubwa mwaka mmoja baadaye, 1976, kwa kuchapwa na Simba mabao 6-0, huku washambuliaji wa Simba Abdalah Kibaden, Jumanne Hassan Masimenti na Willy Mwaijibe wakimyanyasa kipa wa Yanga miaka hiyo Banard Madale.
Lakini kabla ya mgogoro huo, Yanga ilikuwa makini sana, iliweza kutengenisha migogoro ya viongozi na ushiriki wa timu katika michuano mbalimbali.
Ukifanya tathmini, unaweza kuona kwamba pamoja na Yanga kushinda mechi nyingi na kuchukua ubingwa mara nyingi kuliko watani wao Simba, lakini pia idadi ya migogoro iliyoikosesha ubingwa timu hiyo nayo utaona ni mingi pia.
Ndiyo maana katika vikosi vyote vilivyowahi kuwepo Yanga, kuna kimoja chenye majina kama haya ya kipa Elias Michael, Kilambo, Boy Wickens, Hassan Gobos, Omary Kapela, Abdulrahman Juma, Leonard Chitete, Sunday Manara, Kitwana Manara, Maulidi Dilunga na Gibson Sembuli kilichofanikiwa kujenga uimara wa timu na kuwa chenye nidhamu iliyodumu kwa muda mrefu.
Kwa kuwa Yanga hii bado ipo kwenye kumbukumbu ya wapenzi wa klabu hiyo, inabidi mwaka huu 2011 kuirejesha japo kinadharia kwa vile ndiyo iliyokuwa Yanga yenye malengo yaliyokusudiwa tangu ilipoasisiwa mwaka 1935.
Ipo dhana iliyoenea mitaani kwamba migogoro ndani ya klabu za Simba na Yanga hutengenezwa na watu maalum kwa ajili ya maslahi fulani.
Wapo wanaodai kwamba migogoro hiyo ni kazi muhimu na huwa inabadilishwa kutoka timu hizi mbili ili kuisaidia moja na kuididimiza nyingine.
Dhana hiyo inaingia akilini kwa kiasi fulani, kwa vile hutokea migogoro ya timu hizi ikatokea kwa wakati mmoja, kwamba Simba wakorofishane na huku Yanga nao wasiwe na maelewano.
Ila kama imekuwa ikifanyika siyo kwa nia hii ya ubadhilifu, basi kwa Yanga huu si wakati muafaka kwa vile ni kipindi ambacho kugombana baina yao kunaisaidia Simba kuwa juu kisoka mara kwa mara.
Isifikie wakati wenye timu yao (wapenzi) wakaijua siri ya migogoro hii na kisha wakaamua kutumia nguvu kuitatua, tutapoteza maana halisi ya michezo ambayo ni upendo na undugu.
Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa simu namba 0712 328223.
Post a Comment