JIJINI
Simba B yatinga robo fainali
NA EDSON JOEL
LIGI ya vijana chini ya umri wa miaka 20 `Uhai Cup` iliendelea jana katika uwanja wa Karume Dar es Salaam, ambapo timu ya Simba ilitinga hatua ya robo fainali baada ya kuichapa bila huruma African Lyon kwa mabao 4-1.
Mchezo huo ulianza kwa kasi sana huku timu zote zikiwa zimekamiana na kucheza kwa kujiamini pamoja na kuweka tahadhari golini.
Baada ya dakika 18 za mchezo, timu ya Simba ilionekana kucheza kwa nguvu zaidi jambo lililosababisha mshambuliaji wa timu hiyo Kelvin Challe kufunga bao la kwanza katika dakika ya 20.
Bao la pili la Simba lilipatikana katika dakika ya 20 kupitia mshambuliaji wake machachari Kelvin Challe baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Mercel Bonventure.
Mambo yalizidi kuwa magumu kwa timu ya African Lyon baada ya Kelvin Challe wa Simba kufunga bao la tatu katika dakika ya 34 ya kipindi cha kwanza baada ya kuunganisha pasi safi ya Miraji Athuman.
Mshambuliaji huyo wa Simba Kelvin Challe aliendelea kusumbua mabeki wa African Lyon katika kipindi cha pili, ambapo katika dakika ya 71 ya mchezo aliipatia timu yake bao la nne na la ushindi.
Bao pekee la kufutia machozi la timu ya African Lyon lilipatikana katika dakika ya 82 ya mchezo lililofungwa na Abu Mwakasege.
Kwa matokeo hayo Simba ndiyo timu pekee iliyotinga robo fainali bila kupoteza mchezo hata mmoja, ikiwa na pointi 9 na mabao 10.
Majimaji kurejea Januari 13
NA MWANDISHI WETU
TIMU ya Majimaji ya Mjini Songea inatarajia kurejea nchini Januari 13, tayari kwa mzunguko wa pili wa ligi kuu Tanzania Bara inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari 15 mwaka huu.
Timu hiyo iliondoka nchini wiki mbili zilizopita kwenda Msumbiji kwa ajili ya kuweka kambi na kucheza michezo miwili ya kirafiki.
Mchezo wake wa kwanza itacheza na timu ya Nchinga kabla ya mchezo wa pili na Nampula, mchezo utakaofanyika katika uwanja wa Nchiga ambao unatumiwa na timu hiyo kwa ajili ya mazoezi.
Akizungumza na Bingwa kwa njia ya simu akiwa mjini Songea, Makamu Mwenyekiti Ahmed Dizumba alisema timu hiyo ipo katika hali nzuri na matarajiao yao ni kujiweka katika nafasi nzuri zaidi baada ya mzunguko wa pili kuanza rasmi.
“Ukitoa timu za Simba na Yanga kwa ubora bila shaka inayofuata kwa ubora ni Majimaji kwa maana hiyo kuna umuhimu katika mzunguko wa pili wa ligi kuu kudhihirisha kwamba tuna uwezo mkubwa,”alisema.
Berko: Mazoezi ndio suluhisho ya mafanikio
NA TIMZOO KALUGIRA
MLINDA mlango wa timu ya Yanga Yaw Berko, amesema kwamba wachezaji wanatakiwa kufanya mazoezi kwa bidii ikiwa ni pamoja na kumtanguliza Mungu ili waweze kufanya vizuri matika mashindano mbalimbali.
Akizungumza na Bingwa mwishoni wa wiki iliyopita, Berko alisema kuwa wachezaji wengi wa Tanzania wamekuwa na imani za kishirikina, hawapendi kufanya mazoezi.
“Tunahitaji kumtanguliza Mungu katika kazi za mikono yetu, kuliko
kuamini uchawi, nimekuwa nikiona wachezaji na mashabiki wengi wakiona mchezaji akiwekwa benchi anasema kuwa amerogwa lakini mini naamini kwamba unapofanya mazoezi kwa bidii huwezi kukaa benchi,” alisema
Berko alimewashauri wachezaji wa Yanga kufanya mazoezi kwa bidii na kujituma kwa hali na mali badala ya kuamini ushirikiana.
Azam: Tutachukuwa Kombe la Mapinduzi
NA MWANDISHI WETU
KLABU ya Azam FC, imejigamba kuibuka na ushindi katika mashindano ya Mapinduzi Cup.
Akizungumza kwa simu jana, kocha mkuu wa timu hiyo Hall Stewart, alisema kwamba amekuja Tanzania kufanya kazi na siyo kuimba kwaya.
“Nimekuja kuhakikisha naweka historia zaidi ya ile ya kocha mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars, Jan Poulsen, ikiwa ni timu yangu ya taifa ya Zanzibar Heroes na Azam,” alisema Stewart.
Alisema watu wataona maajabu zaidi Azam itakapochukua kombe la Ligi Kuu Tanzania Bara, kwani kikosi chake kiko imara na ndiyo maana wameonyesha mfano nzuri kwenye mashindano ya Mapinduzi kwa kuwafunda Chuoni mabao 3-0 katika mchezo wa ufunguzi.
Alisema kwa sasa anafanya marekebisho katika timu yake kupitia mashindano ya Mapinduzi kabla ya kuanza mzunguko wa pili, ili ahakikishe anazifunga Bingwa mtetezi Simba na timu inayofuata kwa msimamo ya Yanga.
Alisema kuwa katika timu zote zilizoshiriki mashindano ya kombe la mapinduzi hakuna inayomtisha.
“ Bado sijaona timu ya kunisumbua mini, nina wachezaji wazuri wenye uwezo wa kucheza soka,” alisema
Yanga dimbani tena leo
NA TIMZOO KALUGIRA
TIMU ya soka ya Yanga inatarajiwa kushuka tena dimbani leo kupambana na Chuoni katika mchezo wake wa pili wa mashindano ya Kombe la Mapinduzi utakaofanyika katika Uwanja wa Aman mjini Zanzibar.
Katika mchezo wake wa kwanza juzi, Yanga ililazimishwa sare na Zanzibar Ocean View ya kufungana bao 1-1.
Kabla ya pambano hilo, mchana kutachezwa pambano lingine kati ya Azam na Zanzibar Ocean View katika Uwanja huo huo.
Katika mchezo wa leo, Yanga inahitaji ushindi ili iweze kusonga mbele katika mashindano hayo ambayo hufanyika kila mwaka.
Chuoni hadi sasa hawana pointi baada ya kufungwa katika mchezo wake wa kwanza dhidi ya Azam mabao 3-0.
Mashindano hayo yataendelea tena kesho, kwa kuzikutanisha Simba ya Dar es Salaam na KMKM ya Zanzibar, Jioni saa kumi watacheza Mtibwa Sugar ya Turiani Morogoro dhidi ya Jamhuri ya Visiwani Pemba.
Fainali ya shindano la Shujaa Januari 21
NA EDSON JOEL
FAINALI za Shindano la Shujaa wa Safari lager linaloendeshwa na kampuni ya bia Tanzania (TBL), linatarajiwa kufanyika Januari 21mwaka huu Dar es Salaam.
Akizungumza na Waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Meneja bia ya safari lager Fimbo Butallah alisema lengo la shindano hilo ni kutambua mchango wa mashujaa kwa mambo waliyofanya katika jamii inayowazunguka.
Alitaja majina matatu ya mashujaa waliopendekezwa na wananchi kuingia fainali kuwa ni pamoja na Mercy Shayo kutoka Kilimanjaro, ambaye amesaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na vikundi vya akina mama mkoani humo.
Wengine ni Paul Luvinga na Leonard Mtepa wa Dar es Salaam, ambapo Luvinga ameanzisha maktaba yake ambayo usaidia wanafunzi wote kusoma vitabu mbali mbali bure huku Mtepa akiwa amesaidia Bibi Mjane ambaye alitaka kudhulumiwa kwa kumtafutia wakili ili kusimamia kesi hiyo.
`Tulipokea mapendekezo mengi kutoka kwa wananchi wakipendekeza mashujaa wao na mambo waliofanya kwa jamii, ambapo majina hayo yatapigiwa kura na wananchi kulingana na herufi walizopewa Mercy Shayo (A), Paul Luvinga(B) na Leonard Mtepa (C) kwenda namba 15310`alisema.
Mshindi wa kwanza katika shindano hilo atajinyakulia kitita cha shilingi milioni 7 pamoja na milioni 3 kwa ajili ya miradi ya jamii katika eneo analotoka huku wa pili na tatu akiibuka na milioni 1kila mmoja.
BFT kuunda kikosi cha All Afrika Games
NA ONESMO KAPINGA
SHIRIKISHO la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), kimesema wanatarajia kuunda kikosi cha timu ya Taifa itakayoshiriki michezo ya kimataifa ya All Afrika Games, baada ya mashindano ya ubingwa wa Taifa, yatakayofanyika kuanzia Februari 26 hadi Machi 3 mwaka huu, Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana Ofisa Habari wa BFT, Eckland Mwaffisi alisema kuwa mashindano hayo ambayo yatashirikisha timu za mikoa ya Tanzania Bara, mabondia watakaofanya vizuri watachaguliwa kuunda timu hiyo.
Mwaffisi alisema baada ya kocha mkuu wa timu ya Taifa, Mcuba Geovanus Pimenter kuchagua kikosi chake kitaingia kambini haraka kwa ajili ya kujiandaa kimataifa ambao yatafanyika Septemba 3 hadi 18 mwaka huu, Maputo, Msumbiji.
Alisema kuwa mashindano ya taifa yameandaliwa kwa lengo la kupata mabondia watakaojiandaa kushiriki mashindano mablimbali ya kimataifa.
Mwaffisi alisema klabu zitakazoruhusiwa kushiriki ni zile zilifanya mashindano kwa ajili ya kupata wachezaji watakaoiwakilisha klabu yao katika mashindano hayo.
Alisema hadi sasa ni mkoa wa Temeke ambao umefanya uchaguzi wa viongozi na tayari wameshaandaa timu yao baada ya hivi karibuni kufanya mashindano ya mkoa wao.
Mwaffisi alisema mkoa utakaoshindwa kufanya mashindano yake hautaruhusiwa kushiriki mashindano ya Taifa.
Pia ametoa mwito kwa kampuni, mashirika, serikali na watu wenye uwezo binafsi kusaidia maandalizi ya mashindano hayo ili yaweze kufanikiwa kama iliyopangwa.
Post a Comment