ad

ad

MISRI

Stars yatua Misri kiaina

NA MWANDISHI WETU

KIKOSI cha timu ya Taifa, Taifa Stars, kimewasili jijini Cairo, Misri jana mchana na kulakiwa na Watanzania waishio nchini humo.

Stars ipo Misri kwa ajili ya kushiriki michuano ya Bonde la Mto Nile itakayoshirikisha timu za nchi zilizopo katika Ukanda wa Mto Nile, ikiwamo Tanzania.

Katika mchezo wake wa ufunguzi, Stars itaanza na wenyeji Misri kesho, mchezo unaotarajiwa kuwa wa aina yake, Stars ikipania kulipa kisasi cha kufungwa mabao 5-0 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa nchini humo mwaka jana.

Akizungumza na Bingwa kutoka nchini humo, Kocha Msaidizi wa Stars, Sylvester Marsh, alisema kuwa walifika salama na jana jioni walifanya mazoezi tayari kwa mchezo wao wa kesho.

“Tunashukuru tumefika salama na kupokewa vizuri na Watanzania wanaoishi hapa Misri…wenyeji nao wameonekana kutufuatilia kwa karibu ukizingatia tutaanza na timu yao,” alisema.

Akizungumzia mchezo huo wa kesho, Marsh alisema kuwa amewaandaa vyema wachezaji wake, akiwa na imani watacheza vizuri na kushinda.

Mbali na Tanzania na Misri, nchi nyingine zinazoshiriki michuano hiyo iliyoandaliwa na Chama cha Soka Misri (EFA) kwa kushirikiana na serikali ya nchi hiyo, ni Uganda, Sudan, Kenya na Burundi.

Yanga, Chelsea ‘dugu moja’

NA MICHAEL MAURUS

MWENENDO wa timu ya soka ya Yanga katika maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, umeonekana kusuasua kama ilivyo kwa Chelsea ya England katika ligi ya nchi hiyo.

Yanga inayoshika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 25, nyuma ya Simba yenye pointi 27, pia itashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF).

Katika kuhakikisha inatwaa ubingwa wa Bara, ikiwa ni pamoja na kufanya vyema kwenye michuano hiyo ya kimataifa, Yanga ilikiongezea nguvu kikosi chake kwa kusajili wachezaji wawili wakati wa dirisha dogo la usajili ambao ni Mzambia Davies Mwape na Juma Seif ‘Kijiko’ kutoka JKT Ruvu.

Mbali na hilo, timu hiyo ilianza mazoezi mapema, ambayo pia ililenga kuyatumiwa kama maandalizi ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanayoendelea visiwani Zanzibar.

Lakini hadi sasa timu hiyo yenye maskani yake katika makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga, haijaonyesha kiwango cha kuwawezesha kutwaa ubingwa wa Bara, achilia mbali kufurukuta katika michuano ya Kombe la CAF.

Hilo limejonyesha katika mechi za kirafiki za timu hiyo dhidi ya Azam FC ilipofungwa mabao 3-1, dhidi ya AFC Leopards ya Kenya iliposhinda 1-0 pamoja na kuonyesha kiwango duni, kabla ya kulambwa mabao 3-1 na JKT Ruvu wiki iliyopita.

Kama hiyo haitoshi, timu hiyo iliyosheheni nyota wa kigeni, juzi ilitoka sare ya bao 1-1 na Zanzibar Ocean View ya Zanzibar katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi.

Matokeo hayo, hasa dhidi ya JKT Ruvu, yameonyesha kuwavunja nguvu mashabiki wa timu hiyo, japo kocha wa wana-Jangwani hao, Mserbia Kostadin Papic amewatuliza kwa kuwataka wawe na subira, kwa madai kuwa bado anaendelea kukinoa zaidi kikosi chake hicho.

Pamoja na maneno hayo ya Papic, watu wa Yanga wameonekana kukerwa na kila kitu kinachoendelea katika klabu yao ndani na nje ya uwanja, ukizingatia wametumia fedha nyingi kusajili wachezaji wanaolipwa mamilioni ya fedha, hasa wale wa kigeni, lakini hakuna lolote jipya wanalolipata kutoka kwa wachezaji hao zaidi ya kutoka uwanjani vichwa vyao vikiwa chini kila kikosi chao kinaposhuka dimbani.

Hapo ndipio watu wa Yanga wanapohuji usajili wa wachezaji kama Mwape, Waghana Ernest Boakye, Isaack Boakye na Yaw Berko ambaye angalau kazi yake inaonekana anapokuwa golini.

Lakini pia, kiwango kinachoonyeshwa na Yanga, kinazua maswali yaliyokosa majibu kuona timu hiyo inayofundishwa na kocha wa kigeni anayelipwa mamilioni ya fedha inafungwa 3-1 na timu inayonolewa na mzawa anayelipwa ‘vijisenti’ visivyomtoleza hata kumudu kununua pikipiki.

Hakika, hali ilivyo kwa watu wa Yanga kwa sasa, ni kama ilivyo kwa wale wa Chelsea, ambayo kwa sasa imekuwa ikizorota kiasi cha kukatisha tamaa mashabiki wake kama inaweza kutetea ubingwa wake, hata kuwamo katika timu nne za juu England.

Tayari kipa wa Chelsea, Peter Cech ameweka wazi kuwa timu yao hiyo haijawahi kuwa mbovu kama ilivyo sasa baada ya kucheza mechi nane za ligi na kushinda mmoja tu, ikiwa no pamoja na kupokea kipigo cha 3-1 kutoka kwa Arsenal wiki iliyopita na sare ya 3-3 dhidi ya Aston Villa juzi.

Chelsea ya sasa haiwezi kujilinda na hata kushambulia, ikiwa imeacha kufanya mambo waliyokuwa wakifanya mwanzoni mwa msimu wakati walipokuwa hawaruhusu mabao, huku wakifunga mengi.

Hata hivyo, kama wanavyosema wataalamu wa soka kuwa ‘mpira unadunda’, wakiwa na maana kuwa pamoja na mwenendo mbovu wa Yanga, kama ilivyo kwa Chelsea, lolote linaweza kutokea, na haitashangaza Yanga ikitwaa ubingwa wa Bara au Chelsea kutetea ubingwa wake.

Stars yatua kwa mbwembwe Misri

NA MWANDISHI WETU, CAIRO

TIMU ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, imetua

Papic atega bomu

NA ONESMO KAPINGA

KATIKA kinachoonekana kujaribu kukwepa lawama za kufanya vibaya katika michuano ya kimataifa, Kocha wa Yanga, Mserbia Kostadin Papic, ameutaka uongozi wa klabu hiyo kutenga bajeti ya fedha za maandalizi ya michuano hiyo.

Yanga waliokuwa washindi wa pili wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, watashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, yanayotarajiwa kuanza kati ya Januari 28, 29 na 30 mwaka huu.

Yanga itaanza kucheza na Debebit FC ya Ethiopia katika hatua ya awali ya michuano hiyo.

Akizungumza na Bingwa Dar es Salaam juzi, Papic alisema kuwa jukumu lake ni kuandaa timu itakayoshiriki michuano hiyo, lakini hawezi kufanikiwa katika hilo kama viongozi wa Yanga hawatatenga fedha kwa ajili ya maandalizi.

Papic alisema katika kuhakikisha timu inaandaliwa vizuri, ni lazima isafiri na kwenda kucheza mechi angalau tatu za kirafiki za kimataifa, hilo likihitaji fedha.

“Nasubiria viongozi wakitoa bajeti ya maandalizi ya mashindano, ndio niweze kuanza programu zangu,” alisema Papic.

Alisema kuwa ingawa timu hiyo imeanza mazoezi kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, mazoezi hayo hayawezi kukidhi michuano ya kimataifa.

Awali, Papic alisema kuwa anahitaji mechi tatu za kirafiki za Kimataifa kutoka nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ili kikosi chake kiweze kuwa fiti zaidi.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Lloyd Nchunga amekaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa timu hiyo itakwenda kuweka kambi nchini Misri kwa ajili ya kujiandaa na michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho.

Mwisho.

Kayuni ‘akacha’ kukabidhi ofisi TFF

NA ONESMO KAPINGA

KATIBU Mkuu mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Angetile Osiah na Ofisi Habari wake, Boniface Wambura, wameanza kazi jana bila kukabidhiwa nyaraka na aliyekuwa anakaimu nafasi ya ukatibu mkuu, Sunday Kayuni.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Osiah alisema kushindwa kukabidhiwa kwao ofisi kulitokana na Kayuni kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuwasindikiza wachezaji wa timu ya Taifa, Taifa Stars, walioondoka nchini jana kwenda Misri kushiriki mashindano ya Bonde la Mto Nile.

Osiah alisema kuwa walifika ofisini saa 2 asubuhi na kupokewa na Mkurugenzi wa Utawala na Uanachama wa TFF, Mtemi Ramadhan na wafanyakazi wengine wa shirikisho hilo, lakini hadi saa 11 asubuhi, Kayuni alikuwa hajatokea.

“Leo tulitakiwa kuanza kazi na hivyo mmetuona tumekaa, lakini hatujakabidhiwa rasmi ofisi kwani kayuni hayupo,” alisema Osiah.

Alisema kuwa baada ya kukabidhiwa nyaraka za ofisi, atazipitia na kesho ataitisha mkutano wa kwanza na waandishi wa habari kuelezea mikakati yake.

Osiah anakuwa katibu wa pili wa kuajiriwa TFF baada ya kuanzishwa mfumo wa watendaji wake kupewa ajira za kudumu, akirithi mikoba ya Frederick Mwakalebela, huku Wambura akishika wadhifa wake kurithi mikoba ya Florian Kaijage.

Wataka uchaguzi ZFA urudiwe

NA TIMZOO KALUGIRA

WAGOMBEA wawili waliowania uongozi katika uchaguzi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), wamewasilisha rufaa kwa Kamati ya Uchaguzi kupinga matokeo ya uchaguzi, wakitaka urudiwe upya.

Barua hiyo iliwasilishwa jana mjini Zanzibar na aliyekuwa mgombea wa nafasi ya urais, Seleman Mahmud Jabir kwa Mwenyekiti wa Kamati wa Uchaguzi, Alli Seleman Shiata, ilieleza kuwa mgombea aliyeshinda nafasi hiyo, Alli Ferej Tamim, hakuwasilisha cheti cha elimu yake ya kidato cha nne kwa mujibu wa katiba ibara 82 (b).

Barua hiyo ilieleza kuwa wajumbe wa mkutano mkuu wanaotoka katika kamati ya waamuzi, makocha, soka ya wanawake, soka ya vijana na watu wenye ulemavu kutoka Pemba na Unguja, walishiriki katika uchaguzi huo na kupiga kura kinyume cha katiba.

Barua hiyo ilieleza kuwa wajumbe hao, hawakustahili kupiga kura kwani kamati hizo hazikufanya uchaguzi kwa miaka mingi kinyume na katiba zao, ambapo wanahitajika kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mine, kwa mujibu wa katiba ya ZFA ibara ya 32.

Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi, Shiata alikiri kupokea barua hiyo, akisema kamati yake inatarajia kukutana leo kwa ajili ya kujadili rufaa hizo na baadaye watawaita walalamikaji na walalamikiwa kabla ya kutoa uamuzi.

Habari za ndani kutoka ZFA zilizopatikana jana, zilisema uchaguzi huo ni lazima urudiwe kutokana na wadau wengi visiwani humo kutofurahishwa na matokeo hayo kwani walitaka kuwapata viongozi wenye sura mpya.

Kabla ya uchaguzi huo, Amani Makungu ambaye alikuwa anawania nafasi ya makamu wa urais, aliwaambia wajumbe kwamba endapo angeshinda Tamim, angeandika barua ya kujiuzulu.

Baada ya Tamim kushinda, Makungu hadi jana alikuwa hajapeleka barua ya kujiuzulu na watu waliokuwa karibu naye wamesema hatakwenda kwenye ofisi za ZFA na kutoa ushirikiano kwa uongozi huo.

No comments