JIJINI DAR
Habari za Ilala
Na Mohamed Mharizo
Moro kupimana ubavu na Polisi Dodoma
TIMU ya soka ya Moro United inatarajia kucheza na Polisi Dodoma Jumatano kujiandaa na fainali za Ligi Daraja la Kwanza zinazotarajia kuanza Januari 15.
Timu hiyo iliyowahi kucheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara, ilifuzu kucheza fainali hzio baada ya kujikusanyia pointi 15.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hassan Banyai alisema mchezo huo utakuwa muhimu kwa ajili ya kukipima kikosi chake ambacho kimepania kucheza Ligi Kuu msimu ujao.
“Maandalizi yetu yanaendelea vizuri na naamini mchezo huu utaweza kutupa mwelekeo mzuri wa kufanya vizuri,” alisema Banyai.
Timu hiyo kwa sasa inafanya mazoezi katika Uwanja wa Shule ya Msingi Tabata jijini Dar es Salaam.
JM Mbeta kufanya ziara mikoani
BENDI ya muziki wa Dansi ya MJ Mbeta inatarajia kuanza ziara ya mikoani kwa ajili ya kuitambulisha kwa mashabiki wa muziki huo katika kipindi cha mavuno.
Bendi hiyo kwa sasa inafanya maonyesho yake katika Ukumbi wa Panandi uliopo Ilala Bungoni Dar es Salaam chini ya Kiongozi wake Julius Mzeru.
Akizungumza na Mtanzania jana, Mzeru alisema wanatarajia kufanya ziara za mikoani katika kipindi cha mavuno na kwa sasa watakuwa wakipiga kwenye ukumbi huo kila Alhamis.
“Tunahitajia kufanya ziara ya kujitanganza ili kutuweka karibu na wadau wa muziki wa dansi nchini, hivyo tunawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi ili kushuhudia muziki wetu pale Panandi,” alisema.
Aliwataka mashabiki wa muziki wa dansi wawaunge mkono na watawapa burudani ya aina yake na wala hawatowaangusha.
Cosmo kukutana kesho
KAMATI ya Utendaji ya timu ya Cosmopolitan inakutana kesho kwa ajili ya kuhakiki wanachama wake kabla ya Mkutano Mkuu wa wanachama unaotarajia kufanyika Januari 15.
Akizungumza na Mtanzania, Katibu msaidizi wa timu hiyo Baden Msuku alisema mkutano huo utafanyika makao makuu ya timu hiyo Kariakoo.
“Huu ni mkutano ambao utahakiki wanachama ambao watashiriki katika mkutano mkuu, lengo letu ni kuimarisha uongozi katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu,” alisema.
Alisema kwa sasa wanataka kuifanya timu hiyo ili iweze kurejea katika makali yake na kuleta ushindani katika soka kama ilivyokuwa mwaka 1967 ilipoweza kunyakua Ubingwa wa Tanzania Bara.
Pan African yapania ligi
TIMU ya soka ya Pan African ya jijini Dar es Salaam imepania kufanya vizuri katika Ligi ya TFF Mkoa wa Dar es Salaam.
Timu hiyo kwa sasa inafanya mazoezi katika Shule ya Sekondari Azania kwa ajili ya Ligi ya TFF mkoa wa Dar es Salaam chini ya Kocha Mkuu, Likembe Njohole.
Akizungumza jijini jana, Katibu Mkuu wa timu hiyo, Saad Mateo alisema timu inajiandaa vizuri na kwamba lengo lao ni kuleta ushindani zaidi.
“Tunahitaji kurejesha makali yetu kama zamani, tumedhamiria hilo kiukweli,” alisema.
Matola aahidi Ubingwa Kombe la Uhai
KOCHA wa timu ya Simba SC Suleman Matola ameahidi kutofungwa mchezo hata mmoja na kutwaa Ubingwa wa Kombe la Uhai mwaka huu.
Akizungumza mara baada ya mchezo wao na African Lyon ambao waliibuka na ushindi wa mabao 4-1 Matola alisema nia yake ni kuipa timu hiyo Ubingwa wa michuano hiyo mwaka huu.
“Nia yangu ni kuendeleza ushindi kila mchezo na kutwaa ubingwa wa micahuano hii, nashukuru tumemaliza mzunguko wa kwanza bila kupoteza, naamini nitachukua ubingwa”, alisema.
Alisema kutokana na maandalizi mazuri ya kikosi chake anaamini watatwaa ubingwa huo.
Klabu ya baiskeli yaomba udhamini
Na Jennifer Ullembo
KLABU ya vijana ya mafunzo ya baiskeli (GERBA) imewaomba wadhamini kujitokeza kuizamini klabu hiyo vifaa vya mchezo huo .
Akizungumza na Mtanzania, Msemaji wa klabu hiyo Saidi Kengele alisema hadi sasa kilio chao kikubwa ni kupatikana kwa vifaa vya kufanyia mazoezi.
Kengele alisema wanahitaji baiskeli 20 zenye saizi tofauti, mavazi na viatu.
“Kilio chetu ni vifaa tu wadhamini wajitokeze kutusaidia,”alisema Kengele
Msemaji huyo alisema vijana wengi wamekuwa wakipenda michezo nchini lakini wanakwamishwa na vifaa.
“Nimepata vijana wengi wanataka kucheza mchezo huu lakini hakuna vifaa wanapata tabu sana,”alisema Kengele
Kengele alisema michezo ni kitu kizuri nchini kwani inasaidia kuinua vipaji vya wachezaji ambao watailetea sifa nchini yetu katika mashindano makubwa mbalimbali .
Post a Comment