ad

ad
Sasa ni Kili Stars vs Ethiopia

Na Deborah Kajolo

TIMU ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ imefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya kombe la Challenge inayoendelea jijini Dar es Salaam baada ya kuifunga Rwanda bao 1-0.

Kwa matokeo hayo, Stars imetinga hatua ya nusu fainali na sasa itakutana na Ethiopia iliyoanza kutinga hatua hiyo juzi ilipoichapa Zambia mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza wa robo fainali za michuano hiyo.

Katika pambano hilo la jana, mchezo huo ulikuwa mgumu kwa pande zote kwa kila timu kupigana kufa na kupona kuhakikisha inaibuka na ushindi ili kutinga hatua hiyo ya nusu fainali kwani ni hatua muhimu ya kujihakikishia kutinga fainali.

Mchezo huo uliendelea kuwa mgumu kwa pande zote baada ya mvua kubwa kunyesha hivyo mpira kuteleza, lakini ugumu zaidi ulionekana kwa upande wa Kili Stars iliyokuwa inahitaji kuibuka na ushindi nyumbani.

Ndiyo, unaweza kusema Kili Stars ndiyo ilikuwa na wakati mgumu kwa sababu ilikuwa na nia moja tu ya kuhakikisha inaibuka na ushindi ili kutinga hatua hiyo ya nusu fainali lakini ugumu wa mechi hiyo ulizidishwa na matokeo mabaya kwa ndugu zao wa Zanzibar Heroes ambao waliondolewa kwa mikwaju ya penati 5-3 na Uganda katika mchezo uliotangulia.

Bao la Kili Stars lilifungwa na Shadrack Nsajigwa dakika ya 62 kwa njia ya penati iliyopatikana baada ya John Bocco kuangushwa ndani ya 18 na beki wa Rwanda. Hata hivyo Kili Stars itabidi ijilaumu kwa kushindwa kuibuka na ushindi mnono kwasababu ilipata nafasi nyingi na kukosa.

Pengine hilo bado ni lile tatizo sugu la ubutu wa safu yao ya ushambuliaji ambayo inahitaji kufanyiwa marekebisho sana kwani imekuwa ni kama ‘donda’ ndugu lisilo na dawa hali inayowafanya mashabiki kuwa na wasiwasi juu ya ushindi wao kila inapocheza.
xxxxxxMWISHO


Fumo Felician kuongoza msiba wa Nico Bambaga

Na Henry Paul

MCHEZAJI wa Zamani wa Yanga na Pamba ya Mwanza, Fumo Felician leo atawaongoza mamia ya wadau wa soka wakiwapo wachezaji wa zamani kuusindikiza mwili wa mchezaji mwenzao Nicodemus Bambaga ambaye atasafishwa kuelekea Musoma tayari kwa maziko.

Nicodemus alifikwa na mauti juzi katika Hospitali ya Lugalo jijini Dar es Salaam, alikokuwa amelazwa baada ya kuugua maradhi ya mapafu kwa muda mrefu.Nico anayefahamika vema katika nafasi ya kiungo wa ulinzi, atakubukwa na wanasoka hasa klabu ya Pamba, Yanga, Malindi na Simba kutokana na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kutoa pasi za uhakika.

Gazeti la Mtanzania ambalo lilikuwa moja ya mashuhuda waliohudhuria msiba wake nyumbani kwake Kigogo jijini, lilizungumza na wanasoka wenzake wa zamani ambao kila mmoja alionekana kuguswa mno na kifo chake.

“Kwa kweli hili ni pigo, mbele yeye nyuma sisi tunachohitajika kufanya kama kumuenzi mwenzetu ni kuiga uwezo wake wa uchezaji na hili ni jambo linalopaswa kufanywa na wachezaji wa sasa,” alisema Fumo Felician.

Fumo anasema ameguswa sana na kifo cha Nico kwa sababu alikuwa ni rafiki yake wa karibu ambaye walisajiliwa msimu mmoja Yanga mwaka 1993. Naye Sekilojo Chambua aliungana na Fumo kwa sababu wote walisajiliwa Yanga mwaka huo huo.

Lakini kwa upande wake Sekilojo Chambua, alisema ameguswa sana na anaungana na familia yake pamoja na wanasoka kwa ujumla katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo, “Pengo lake kwangu halitazibika, alikuwa zaidi ya rafiki kwasababu tulisajiliwa pamoja Yanga yeye akitokea Pamba mimi Tukuyu lakini pia tulikuwa wote mwaka 1992 katika kikosi cha timu yetu ya Taifa ‘Tafa Stars.

Naye Willy Martin, alisema bado kivuli cha Bambaga kitaendelea kumfuata kwa sababu walifahamiana vema kwa kucheza pamoja mara mbili, mosi Willy alipokuwa Ushirika Moshi na Bambaga Pamba na mara ya pili walipokuwa pamoja Yanga walipofanikiwa kuwachapa watani wao wa jadi Simba mabao 4-1 mwaka 1994.

Anasema katika mchezo huo ndio utamfanya aendelee kumkumbuka kwa sababu alikuwa anatoa pasi nzuri na uhakika bila kuchoka. James Washokera anamkumbuka walipocheza wote Pamba, Bambaga akicheza namba tano na yeye (Washokera) sita alikuwa akiwasaidia sana. Juma Mgunda hatamsahau Bambaga walipokutana wakati yeye akichezea Coast Union ya Tanga alikuwa akiwapa tabu sana. Naye Offen Martin hata msahau alivyokuwa akiwasumbua kila timu zao zilipokutana wakati huo Offen akichezea Ushirika Moshi.

Nico Bambaga atakumbukwa vema na familia ya soka hasa akiwa nahodha wa kikosi cha timu ya taifa kilichobeba kombe la Challenge nchini Kenya mwaka 1994. Marehemu ameacha mjane na motto mmoja.
xxxxxxxMWISHO

No comments