ad

ad
Makungu: Kombo ataboresha soka Zanzibar

Na Mwandishi Wetu

MMILIKI wa hoteli yenye hadhi ya kimataifa ya Zanzibar Ocean View, Aman Makungu amesema endapo atafanya kazi katika Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) na Mahmoud Thabit Kombo soka la Zanzibar litakuwa la kimataifa.

Makungu aliyepanga kuwania nafasi ya Makamu wa Rais wa ZFA, bado hajachukua fomu akisubiri kwanza swahiba wake huyo aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Zanzibar achukue fomu ya Urais wa chama hicho.

Mfanyabiashara huyo alisema anaamini kufanya kazi na Kombo ZFA kutaleta maendeleo makubwa katika soka kwani kwa pamoja wanaamini soka la Zanzibar ili likue linahitaji kuedeshwa kisayansi zaidi.

“Naamini safu yangu na Kombo na viongozi wengine watakaochaguliwa katika uchaguzi huo tutafanya kazi kwa uhakika na soka la Zanzibar litakuwa mno tofauti na ilivyo sasa na hata ule uanachama wa Fifa tunaousotea kuupata mpaka sasa utapatikana,” alisema Makungu.

Alisema swaiba wake huyo, Kombo anataka nafasi hiyo kwa lengo la kumtoa Ali Fereji Tamim aliyekaa madarakani miaka 20 pasipo mabadiliko yanayotakwa na Wazanzibar.

Alisema endapo Kombo hatachukua fomu hiyo, hata yeye hatagombea nafasi hiyo ya Makamu wa Rais wa ZFA wala nafasi yeyote kwani anaamini wale waliyoazimia kuyafanya hayatatimia.

“Tukifanikiwa kuwa madarakani tutaajiri katibu mkuu mwenye sifa za kimataifa kutoka Ulaya, mhasibu mwenye sifa tofauti na ilivyo sasa kwani wakati mwingine katibu wa ZFA anafanya kazi za mhasibu,” alisema Makungu.

Alisema lengo lao lingine la maendeleo ya ZFA ni kutaka kujenga jengo kubwa la chama hicho lenye ofisi zenye hadhi ya chama hicho.

Waliochukua fomu za kuwania nafasi ya Makamu wa Rais mpaka sasa ni Hadji Ameri anayetetea nafasi ya cheo chake hicho, Ibrahim Raza aliyewahi kushika nafasi hiyo miaka ya nyuma na Yusuph Omary Chunda.

ZFA wanatarajia kufanya uchaguzi mkuu wa viongozi, Desemba 31 mwaka huu Kisiwani, Pemba.


xxxx

Taifa Queens yaendeleza dozi Singapore

Na Jennifer Ullembo

TIMU ya Taifa ya netiboli ‘Taifa Queens’ juzi iliendeleza kugawa dozi baada ya kuinyuka India mabao 62 -27.


Akizungumza na Mtanzania jana Katibu Mkuu wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA), Anna Bayi alisema mchezo huo ulikuwa mgumu na timu zote zilionesha ushindani mkubwa.
.
Bayi alisema Taifa Queens ilijitahidi kuhakikisha haifungwi katika michezo iliyobakiza.

“Mchezo ulikuwa mgumu lakini timu yetu ilionyesha uwezo wa hali ya juu na kuleta ushindani mkubwa hasa ukizingatia wenzetu wana wachezaji wazuri,” alisema Bayi.


Bayi alisema mbali na Taifa Queen kuanza kufanya vibaya katika ufunguzi wa mashindano hayo hali ilibadilika pale Taifa Queens ilipocheza na wenyeji wa mashindano Singapore na kuibuka na ushindi wa mabao 52 -36.

Aliwaomba Watanzania kuiombea timu hiyo iliiweze kufanya vizuri kwani itashuka dimbani leo kukipiga na Namibia.

Michauno ilyoanza kutimua vumbi Desemba sita nchini Singapore, inatarajiwa kufika tamati Desemba 12.
xxxxxxxxMWISHO


Coastal Union Kambini Desemba 13

Na Jennifer Ullembo

TIMU ya Coastal Union inatarajiwa kuingia kambini Desemba 13 mkoani Tanga ikiwa na kikosi cha wachezaji 30.

Akizungumza na Mtanzania jana, Mwenyekiti wa kamati ya usajili wa timu hiyo Ahmed Aurora alisema kwa sasa wanaendelea kuuguza wachezaji wao wa tatu ili nao waweze kujiunga na wenzao kambini.

Aurora aliwataja wachezaji wanaoumwa ni Peter Fea aliyepata jiraha la kifundo cha mguu, Endry Mngoma na Msile Shaffy wote hao wanaugulia maumivu ya goti.

“Wachezaji wanaendelea vizuri na anaimani watakuwa safi kuingia kambini na wenzao Desemba 13,”alisema Aurora.

Alisema kwa sasa wanajipanga kuleta maangamizi mzunguko wa pili wa ligi daraja la kwanza unaotarajiwa kuanza kutimua vumbi Desemba 27.

xxxxxxxxMWISHO

Simba waombwa kuhamia Mkwakwani

Na Mohamed Mharizo

WANACHAMA na mashabiki wa Simba mkoani Tanga wameitaka timu yao kutumia uwanja wa Mkwakwani kama uwanja wao wa nyumbani wakati wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom itakayoanza Januari 15.

Akizungumza na Mtanzania kwa niaba ya wanachama, mwenyekiti wa matawi ya Simba mkoani humo, Mbwana Msumari alisema.

“Sisi wanachama wa Simba mkoani Tanga tunawaomba viongozi wetu kusikiliza ushauri huu kwa kuwa huku wanachama ni wengi kuliko Mwanza.

“Hata mapato yanayopatikana timu ikicheza Mkwakwani ni makubwa kuliko Mwanza,” alisema Msumari.

Alisema faida ya timu hiyo kutumia uwanja huo ni kubwa kwani ina mashabiki wengi Tanga na pia mashabiki wengi wanaweza kufika mkoani humo kutokana na jiografia ya mkoa huo tofauti na ule wa Kirumba.


Gazeti la Mtanzania liliamua kuwatafuta viongozi wa Simba akiwemo mwenyekiti wake timu hiyo, Ismail Rage ili kuzungumzia suala hilo ambaye alisema yuko porini hawezi kuzungumza.

Jitihada za kuwapata hazikuzaa matunda kwani alipotafutwa Makamu Mwenyekiti Geofrey Nyange ‘Kaburu’ kwa simu yake ya kiganjani muda wote iliita bila kupokelewa.

Jitihada za Mtanzania kuwatafuta viongozi hao zilikuwa zinahitaji kufahamu jinsi watakavyokubaliana na wanachama pamoja na timu ya Azam FC ambayo tayari imeshatangaza kutumia uwanja huo pamoja na kuufanyia ukarabati.

Ukarabati huo ulifanyika Novemba 26 na unatarajiwa kuwa tayari kwa matumizi kuanzia Januari 14 utakapofunguliwa rasmi kwa ajili ya duru la pili la Ligi Kuu.
xxxxxxxMWISHO

No comments