ad

ad

Utafiti mpya kwa vijana wa miaka 15 – 24 kuhusu fedha na simu.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Well Todl Story inayoendesha kampeni ya Shujaaz, Rob Burnet akizungumza na vijana mbalimbali katika mkutano uliojadili fursa mbalimbali kwa vijana uliofanyika Dar es Salaam.
Takwimu zinaonesha FURSA mbalimbali kwa vijana wa Tanzania.
NUSU ya vijana wenye miaka 15 mpaka 24 nchini Tanzania, wamesema hawana fedha za kutosha kutimiza mahitaji yao ya kila siku, kwa mujibu wa utafiti mpya uliochapishwa jijini Dar-es-salaam leo (Jumatano tar 22 Juni), na kampuni inayozalisha vipindi vya redio, machapisho, na uendeshwaji wa mitandao ya kijamii iitwayo Well Told Story. Takwimu hizo pia zinaonesha kuwa vijana nchini Tanzania hutumia kwa wastani mara tatu zaidi ya kiasi wanachoingiza kila mwezi, wakiwa tegemezi kwa wazazi au watu wengine katika kuwatimiza mahitaji yao.

Tafiti hiyo inaonesha kuwa zaidi ya nusu ya vijana wa Tanzania, huishi kwa mipango ya kila siku isiyo endelevu, huku wakiendelea kutafuta mbinu zaidi za kuingiza fedha. Hata hivyo, simu ni kitu muhimu sana kwa kijana wa Tanzania na kwa wastani, kijana hutumia angalau theluthi ya kipato chake cha mwezi kwenye simu. Vijana wengi wa kiume huanza kuingiza kipato tangu wakiwa na miaka 11 – 13.

Takwimu hizo pia zinaonesha kuwa fursa za ajira, hasa kwa wasichana, ni chache na si rahisi kupatikana. Ripoti inasema wasichana mara nyingi hutegemea wapenzi wao au waume zao (kwa walioolewa) kwa ajili ya kujikimu kimaisha, pia mmoja (1) kati ya wasichana saba (7) mijini na mmoja kati ya wasichana watano (5) vijijini kupata mimba katika umri mdogo.

Ripoti hii ya kina kuhusu vijana wenye umri wa miaka 15 – 24 imezinduliwa rasmi mjini Dar-es-salaam. Ripoti hii ni ya aina yake na ni ya kwanza kujaa uchambuzi wa kina kuhusu mitazamo ya vijana juu ya maisha, mapenzi, vyombo vya habari, ajira, kilimo na fedha. Kwa mujibu wa ripoti hii iliyopewa jina la #Shujaaz360, kukosekana kwa uhakika wa fedha, hutawala kwa kiasi kikubwa mienendo ya maisha ya vijana. Kwa kijana Mtanzania, kila kitu kinachomzunguka au anachohitaji kukifanya lazima kiwe kinahusu fedha. Ripoti hii inatarajiwa kubadilisha mtazamo wa jinsi ambavyo serikali, asasi mbali mbali, sekta binafsi na mashirika ya umma, zinavyojishughulisha na vijana.

Allan Lucky, mtayarishaji wa vipindi na machapisho wa Well Told Story, anasema:

"Kama unahitaji usikivu wa vijana wa Kitanzania, basi utahitaji kuwasiliana nao kwa njia ambayo wanaikubali na itawagusa moja kwa moja. Kutokana na utafiti wetu, ni wazi kwamba mawazo ya vijana wa kisasa Tanzania, yanaongozwa na utafutaji na upatikanaji wa fedha kirahisi & kwa haraka. Kama ukifanikiwa kuwasaidia kupata ushauri na dondoo mbali mbali au taarifa zinazohusu upatikanaji wa fedha kirahisi & kwa haraka, basi utakuwa umekamata usikivu wao."

Mwezi uliopita, Well Told Story ilizindua ripoti kama hii jijini Nairobi, kuhusu vijana wenye umri wa miaka 15 mpaka 24 nchini Kenya, na wadau mbali mbali waliipokea vizuri kwa ajili ya mipango yao ya kila siku juu ya vijana. Ripoti ya Kenya ilisababisha mazungumzo yasiyo na mwisho kupitia mitandao ya kijamii ambapo kwa muda mfupi hashtag ya #Shujaaz360 iliingia miongoni mwa mada kuu za mazungumzo kwenye Twitter, yaani trending topics, na pia kurasa za mbele za magazeti na vyombo vingine vya habari viliizungumzia kwa siku kadhaa zilizofuata.

Well Told Story ni kampuni iliyoanzisha mradi ulioshinda tuzo za kimataifa za Emmy (International Emmy Awards) kwa ajili ya vijana ujulikanao kama Shujaaz, mradi unaojumuisha machapisho ya kila mwezi, vipindi vya redio vya kila wiki na majadiliano makubwa kwenye mitandao ya kijamii kila siku. Mradi huu ulizinduliwa mwezi Machi mwaka 2015 nchini Tanzania, na simulizi zake hufikia mamilioni ya Watanzania vijana kupitia majukwaa mbalimbali ya habari.

o   Nakala zaidi ya 500,000 za majarida ya bure hugawanywa kila mwezi kupitia mtandao mpana wa wauzaji wa Coca-Cola na gazeti la Mwanaspoti.

o   Kipindi cha redio cha kila wiki kupitia vituo mbali mbali vya redio, vikiwemo TBC FM, East Africa Radio, Chuchu FM na Kings FM.

o   Mitandao mbali mbali ya kijamii ambayo maelfu ya vijana wanajiunga kwa ajili ya majadiliano kuhusu mada mbali mbali.

No comments