| WACHEZAJI wa
mchezo wa pool nchini wametakiwa kutumia mchezo huo kama sehemu ya ajira
kwao na pia sehemu ya kukukutana na
kupeana mawazo ya kuinuana kimaisha.
Hayo yalisemwa
mjini hapa jana na Katibu Tawala wa
Wilaya ya Moshi Mjini,Remida Ibrahim wakati wa ufunguzi rasmi wa fainali za taifa za mashindano ya ‘Safari
Lager National Pool Championship 2014’, zinazofanyika kwenye ukumbi wa Kuringe ambapo
yeye alikuwa mgeni rasmi akimwakilisha Mkuu wa wilaya hiyo, Ibrahim Msengi.
Bw. Ibrahim
amesema mchezo huo kwa sasa ni ajira kwa wanaoucheza, hivyo ni vema wachezaji
wakautumia vizuri kwa ajili ya kuwainua kimaisha badala ya kuutumia kwa masuala
ambayo hayana faida katika maisha yao.
“Nitumie
nafasi hii kukushukuruni wadhamini wa mchezo huu kwa kupitia bia ya Safari lager kutokana na
kwamba umeongeza ajira kwa vijana, hivyo wachezaji niwasihi tumieni mchezo wa
pool kuweza kuinua maisha yenu na pia mnapokutana katika mashindano kama hayo
tumieni nafasi hii kushauriana masuala ya msingi ya kuwainua kimaisha,”alisema
Ibrahim.
Anasema kazi
kubwa iliyofanywa na wadhamini wa mchezo huo ni kubwa ambayo inatakiwa kuigwa
na makampuni mengine katika kuinua michezo nchini na pia kuibua ajira kwa
vijana.
Ibrahim
anasema endapo wachezaji watautumia kama ilivyo lengo la mdhamini la kuuinua na
kuupandisha chati kuna uwezekano mkubwa ukailetea sifa Tanzania katika
mashindano ya Afrika.
Alisema
mwaka jana timu ya taifa iliweza
kuthubuti katika mashindano ya Afrika kwa kushika nafasi ya tatu huku mchezaji
Patrick Nyangusi akiibuka bingwa wa Afrika kwa upande wa mchezaji mmoja mmoja
(wanaume).
“Kwa kweli
niwapongeze kwa kazi hiyo kubwa ya kutuwakilisha vizuri katika mashindano hayo
na nina imani mkiendelea hivi kuna uwezekano mkubwa mkatutoa kimasomaso kwa
kuchukua ubingwa wa Afrika, hivyo wachezaji ni kazi kubwa kuzidisha nidhamu na
mazezi maana bila ya nidhamu hakuna mafanikio yayoweza kupatikana,”akasema.
Naye menaja
wa bia ya Safari Lager, Oscar Shelukindo wakati akizungumza kwenye ufunguzi huo aliwataka
wachezaji wa timu zote zinazoshiriki fainali hizo kucheza kwa utulivu hadi
mwisho wa fainali hizo.
Shelukindo alisema
haitakuwa jambola busara endapo fainali
hizo zitamalizika huku wakiacha gumzo la vitendo ambazo si vya kiungwana.
“Kwanza niwape
pole kwa uchovu wa safari ndefu mlikotoka kwenye mikoa yenu kwa ajili ya kufika
hapa kushiriki fainali hizi lakini niwombe tucheza kwa amani bila ya kufanya
jambo lolote la kuashiria vurugu na tukitoka hapa tuache simulizi nzuri mkoani hapa,”alisema Shelukindo.
Amesema wao
kama wadhamini wa mchezo huo hawatapenda kuona nidhamu mbovu kwenye mchezo huo
ambao sasa umekuwa ni mmoja wa michezo tishio nchini.
“Tucheze
vizuri kwa kufuata sheria na kanuni za mchezo huu hadi mwisho ili uendelee
kupendwa kama ulivyo sasa,”amesema.
Makamu
mwenyekiti wa chama cha mchezo huo taifa (TAPA), Fredy Mush licha ya
kuwapongeza wadhamini bia ya Safari Lager kwa kuutoa mbali lakini pia ameelezea
kuridhishwa na viwango vya wachezaji wa timu zote 17 zilizoshiriki fainali hizo.
Mushi
amesema kila mwaka viwango vya wachezaji vinaongezeka hali inayowapa imani ya
kuwa mchezo huo sasa ni tishio nchini.
“Kwa kweli
mchezo wa pool umefika pazuri maana kila mwaka tunashuhudia viwango vya
wachezaji vikipanda hali inayoonyesha kuwa kuwa mchezo upo juu,”amesema Mushi.
Kabla ya
fainali hizo kufunguliwa rasmi wachezaji
na viongozi wa chama cha mchezo huo taifa (TAPA) pamoja na meneja wa bia
ya Safari Lager, Osacr Shaelukindo walitembelea wagonjwa katika hospitali ya Rufaa ya Mawenzi ya mkoa wa Kilimanjaro na
kutoa zawadi mbalimbali kwa wagonjwa.
Akizungumza
baada ya wachezaji na viongozi wa TAPA kumaliza kutembelea wodi ya akinamama
waliokwishajifungua na ambao hawajajifungua na wodi ya watoto,Kaimu Afisa
Muuguzi Mkuu na Msimamizi Wodi ya
Wazazi, Fatima Rashid aliushukuru ugeni huo na kudai ni mfano wa kuigwa na
vijana wengine.
“Kama
mnavyojua wengine hapa hawana ndugu hivyo kuja kuwatembelea na kuwatelea zawadi
kama hivi ni jambo zuri la kuigwa na wengine kwa kujenga tabia ya kutembelea
kuwaona wagonjwa,”akasema Rashid
Timu zilizoshiriki
fainali hizo na mikoa yao ikiwa kwenye mabano ni Blue Leaf (Lindi), Bilele
(Kagera), Mpo Afrika (Temeke), Mashujaa (Ilala), Topland (Kinondoni), Yakwetu
(Pwani), Billiard (Mwanza) na New Stend
(Shinyanga).
Nyingine ni Delux (Dodoma),Black Point (Mbeya), Ngarenaro
(Arusha), Nginja Master (Iringa), Corner Kasara (Manyara), Absom (Tanga), Anatory (Morogoro), Tiptop (Tabora) na
wenyeji Mboya (Kilimanjaro).
|
Post a Comment