MALINZI, NYAMLANI WATAKA URAIS TFF
.
HARAKATI za kuwania urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) sasa
zimeanza kushika kasi baada ya wanamichezo wawili maarufu nchini
kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo.
Wanamichezo hao, Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF, Athumani Nyamlani na
Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoa wa Kagera, Jamal Malinzi walichukua
fomu hizo jana.
Mgombea mwingine aliyechukua fomu jana kwa ajili ya kuwania nafasi hiyo
ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoa wa Kigoma, Omari Mussa Nkwarulo.
Malinzi alichukua fomu ya kuwania nafasi hiyo kwa njia ya mtandao na
kuirejesha jana, akiwa ameambatanisha ada ya sh. 500,000 wakati Nyamlani
alichukua fomu hiyo katika ofisi za TFF na kuijaza papo hapo kabla ya
kuirejesha.
Malinzi aliwahi kuwa katibu mkuu wa klabu ya Yanga mwishoni mwa miaka ya
1990 na pia aliwahi kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi wa mwaka 2008,
lakini alipigwa mweleka na rais wa sasa wa TFF, Leodegar Tenga.
Kwa upande wake, Nyamlani amewahi kuwa katibu wa Chama cha Soka wilaya
ya Temeka (TEFA) na pia katibu wa Chama cha Soka mkoa wa Dar es Salaam
(DRFA).
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alisema jana kuwa, hadi sasa
jumla ya wagombea 30 wamechukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali za
uongozi wa shirikisho hilo.
Akizungumza baada ya kurejesha fomu yake, Malinzi alisema anampongeza
Tenga kwa kufanya maamuzi magumu ya kutogombea tena nafasi hiyo.
Malinzi alisema hali hiyo inawafanya wapiga kura watakaoshiriki katika
uchaguzi huo kufanya maamuzi sahihi kwa kumchagua kushika nafasi hiyo
kwa vile ana uwezo wa kuliongoza shirikisho hilo.
"Naaamini kuwa wapiga kura watakuwa na imani na mimi kwani si mara yangu
ya kwanza kuomba nafasi hii, niliomba mwaka 2008, lakini kura
hazikutosha," alisema Malinzi.
Naye Nyamlani alisema ameamua kuwania nafasi hiyo kwa lengo la
kuendeleza soka ya Tanzania, kazi iliyokuwa ikisimamiwa vyema na Tenga,
ambaye yeye ni msaidizi wake mkuu.
"Nadhani mimi ndiye ninayefaa kuendeleza kazi hiyo na iwapo
nitachaguliwa, nitaifanyakazi hiyo kwa umakini mkubwa na kutilia mkazo
programu ya kuendeleza soka ya vijana,"alisema Nyamlani, ambaye
alisindikizwa na kundi kubwa la wapambe
Mgombea mwingine aliyechukua fomu jana ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira
wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA), Elias Mwanjala anayewania ujumbe wa
Kamati ya Utendaji ya TFF kuwakilisha Kanda ya Iringa na Mbeya.
Orodha kamili ya wagombea waliochukua fomu ni Athumani Nyamlani, Jamal
Malinzi na Omari Nkwarulo (urais), Michael Wambura, Ramadhan Nassib na
Wallace Karia (umakamu wa rais).
Wanaowania ujumbe wa Kamati ya utendaji, kanda zao katika mabano ni
Salum Chama (Kagera na Geita), Mugisha Galibona, Samuel Nyalla, Titus
Osoro na Vedastus Lufano (Mara na Mwanza), Epaphra Swai na Mbasha Matutu
(Shinyanga na Simiyu), Charles Mugondo na Elly Mbise (Arusha na
Manyara), Yusuph Kitumbo (Kigoma na Tabora), Ayubu Nyaulingo, Nazarius
Kilungeja na Selemani Kameya (Katavi na Rukwa).
Wengine ni James Mhagama (Njombe na Ruvuma), Athuman Kambi (Lindi na
Mtwara), Hussein Mwamba na Stewart Masima (Dodoma na Singida), Farid
Nahdi na Twahili Njoki (Morogoro na Pwani), Elias Mwanjala (Iringa na
Mbeya), Khalid Mohamed (Kilimanjaro na Tanga) na Muhsin Balhabou,
Shaffih Dauda na Zafarani Damoder (Dar es Salaam).
Mgombea wa nafasi ya Urais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini TFF. Othumani Nyamlani (kulia) akichukua fomu ya kugombea nafasi hiyo Dar es salaam jana kwa mmoja wa maofisa wa TFF. Jonathan Kakwaya Dar es salaam leo mwingine ni Mwenyekiti wa chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya, Elias Mwanjara.Picha na www.burudan.blogspot.com |
Mgombea wa nafasi ya Urais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini TFF.Jamal Malinzi (kulia) akiludisha fomu ya kugombea nafasi hiyo Dar es salaam leo kwa mmoja wa maofisa wa TFF. Jonathan Kakwaya. Dar es salaam jana.Picha na www.burudan.blogspot.com |
Post a Comment