ad

ad

Miaka 17 ajali ya ndege, Zambia bado kiwango




Rais wa chama cha Soka Zambia ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Kalusha Bwalya (Kushoto) na wachezaji wa timu hiyo wanaoshiriki michuano ya CECAFA inayoendelea jijini Dar es Salaam.
Mohamed Mharizo

MICHUANO ya Kombe la Challenge inafanyika jijini Dar es Salaam ikishirikisha jumla ya nchi 12 kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.


Timu hizo shiriki ni pamoja na wenyeji Kilimanajro Stars, Zanzibar Heroes, Zambia, Burundi, Somalia, Rwanda, Ivory Coast, Sudan, Uganda, Kenya, Malawi na Ethiopia.


Lakini binafsi huwa napatwa na huzuni na kukumbuka mbali zaidi, pindi ninapoiona timu ya taifa ya Zambia, ni ile ajali mbaya ya ndege iliyoua viongozi na wachezaji wa timu hiyo Aprili 27, 1993.

Ndege hiyo ilianguka kwenye Bahari ya Atlantic mara baada ya kutoka Uwanja wa Ndege wa Gabon ilipokuwa njiani kuelekea Senegal.

Katika ajali ile mbaya, hakika Zambia ilipoteza wachezaji mahiri ambao kamwe hawatosahaulika katika vitabu na makumbusho ya taifa hilo.

Wachezaji waliopoteza maisha katika ajali ile ni makipa Richard Mwanza na Efford Chabala, mabeki Whiteson Changwe, Samuel Chomba, Kenan Simambe, John Soko, Robert Watiyakeni na Winter Mumba.

Washambuliaji walikuwa EstonMulenga, Derby Makinka, Moses Chikwalakwala, Wisdom Mumba Chansa, Godfrey Kangwa, Numba Mwila, Kelvin ‘Malaza’ Mutale, Timothy Mwitwa, Moses Masuwa na Patric ‘bomber’ Banda.

Viongozi waliopoteza maisha wakiwa na timu hiyo ni Godfrey ‘Ucar’ Chitalu, aliyekuwa kocha wa timu hiyo na mchezaji wa zamani wa Zambia.

Mara baada ya maafa yale, kiliundwa kikosi kipya na Kalusha Bwalya, mchezaji nyota wa nchi hiyo na Rais wa Chama cha Soka Zambia, alichaguliwa kuwa nahodha wa timu hiyo iliyoshiriki fainali za Kombe la Dunia, hata hivyo walitolewa kwa kufungwa 1-0 na Morocco.

Ni miaka 17 sasa tangu ajali ile itokee, ajali ambayo ilitikisa soka la Afrika na dunia kwa ujumla na kuacha simanzi, vilio na huzuni kwa wananchi wa Zambia.

Pamoja na kupoteza nyota hao, Zambia ilifanikiwa kushiriki Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1994, ambazo fainali zake zilifanyika nchini Tunisia, ilikuwa ikimjumuisha Bwalya.

Kikosi hicho kilifanikiwa kutinga fainali na kupambana na Nigeria, hata hivyo kilifungwa 2-1 na wababe hao na kutwaa kombe hilo.

Bwalya mara baada ya maombolezo ya mwezi mmoja, aliwahi kusema;
“Nimepata majeraha ya moyo yasiyopona maisha, nitakwenda nayo kaburini.

“Nimepoteza ndugu na rafiki zangu wakubwa wa soka namna ile, inaniuma, nitawakumbuka wakati wote wa furaha na huzuni”.

Hakuna ubishi kuwa Bwalya ndiye mchezaji pekee aliyeweka historia ya nchini humo na bado ataendelea kuwa katika vitabu vya kumbukumbu na makumbusho kutokana na mchango wake akiwa mwanasoka na wadhifa wa juu wa uongozi.

Bwalya aliwahi kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa soka wa Bara la Afrika mwaka 1988, akitanguliwa na Rabar Madjer wa Algeria (1987) na kufuatiwa na George Weah wa Liberia (1989).

Si hivyo tu, pia mchezaji huyo aliwahi kushika nafasi ya 14 katika kinyang’anyiro cha kuwania uchezaji bora wa soka duniani mwaka 1996, katika uchaguzi wa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA).

Katika kinyang’anyiro hicho, mshambuliaji wa Brazil , Romario De Souza Faria, alinyakua nafasi ya kwanza, huku nafasi ya pili ikishikwa na Roberto Baggio wa Italia.

Timu ya taifa ya Zambia sasa iko jijini Dar es Salaam ikishiriki michauno ya Challenge, huku Bwalya akiwa ndiye Rais wa chama cha soka nchini humo.

Tayari Zambia imeonyesha kiwango kizuri kwenye michuano hiyo baada ya kuwafunga wenyeji Kilimanjaro Stars 1-0 na kutoka sare na Burundi.

Hapana shaka kuwa kizazi kile cha wachezaji waliopoteza maisha katika ajali ile mbaya ya ndege bado kipo.

Kwa sasa Bwalya ni mchezaji pekee wa kizazi kile ambaye hadi leo ndiye shujaa wa Zambia.Alizaliwa katika mji wa Mafulira mnao mwaka 1959.

Huwezi kulizungumzia soka la Zambia bila kuwzungumzia mashujaa wa ajali ile ya ndege, Rais wa Kwanza wa nchi hiyo Kenneth Kaunda na Bwalya pia.

No comments