ad

ad
Kuiona Challenge sasa Sh 1,000

Na Jennifer Ullembo

SHIRIKISHO la Soka (TFF), limetangaza viingilio vya mechi za robo fainali na nusu fainali katika michuano ya Kombe la Challenge, itakayoanza kutimua vumbi leo, huku kiingilio cha chini kikipangwa kuwa Sh 1,000 na cha juu Sh 5,000.

Leo kutakuwa na michezo miwili kati ya timu ya Zambia na Ethiopia mchana, na jioni ni Ivory Coast ikionyeshana kazi na Malawi, michezo yote itachezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Sunday Kayuni, alisema wanaamini viingilio hivyo, vikiwamo vile vya Sh 2,000 jukwaa la Orange na Sh 4,000 (VIP B), vitawapatia burudani kamili wapenda michezo, hasa wa mpira wa miguu.

“Katika viti vya VIP B, pia kutakuwa na viti 400 maalumu kwa waandishi wa habari, waamuzi na wadau wengine wanaostahili kuangalia mechi hizo kwa ushirikiano wao mzuri kwetu.

“Naamini wadau na mashabiki wa soka hapa nchini watavipokea vizuri viingilio hivyo kwa maslahi ya mpira wa miguu,” alisema.

Uamuzi huo wa TFF ni mwendelezo wa kauli ya Rais wao, Leodger Tenga, ambaye aliamua kuondoa viingilio wakati wa hatua za makundi na kuruhusu mashabiki kuingia bure, jambo lililosaidia mashabiki walioingia kwa wingi kuishangilia Kilimanjaro Stars, ilipomenyana na Burundi na kuichapa 2-0 hivyo kutinga hatua ya robo fainali.

Michuano hiyo iliyoanza kutimua vumbi Novemba 27, imeshirikisha timu 12 kutoka nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ambayo itafikia kilele Desemba 12.
xxxxxxxxxxMWISHO

Nani zaidi Zambia au Ethiopia leo?
Na Mwandishi Wetu

VINARA wa kundi A, timu ya Taifa ya Zambia ‘Chipolopolo’ leo inashuka dimbani kumenyana na Ethiopia katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya michuano hiyo inayoanza leo.

Mchezo huo unasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini, kutokana na uwezo mkubwa wa timu hizo katika hatua ya makundi, lakini jicho zaidi ni kwa Chipolopolo, ambayo imetinga hatua hiyo bila kupoteza mchezo wake katika hatua ya makundi.

Chipolopolo iliyokuwa kundi A na Kilimanjaro Stars, Somalia na Burundi, ilijikusanyia pointi saba baada ya kuibuka na ushindi ilipocheza na Kili Stars na Somalia, huku ikilazimishwa suluhu na Burundi. Burundi wao wametinga nafasi hiyo baada ya kushika nafasi ya pili kutoka kundi C.

Michezo mingine ya robo fainali inatarajia kuendelea kesho kwa wenyeji Kili Stars kushuka dimbani kuonyeshana kazi na Rwanda, mchezo ambao matokeo yake yanasubiriwa kwa hamu, hasa na mashabiki wa hapa nchini ambao wanapenda kuiona Stars ikitinga nusu fainali.
xxxxxxxxMWISHO

Wachezaji Simba wagomea mazoezi

Na Deborah Kajolo

WACHEZAJI watano wa Simba wamekacha mazoezi ya viungo ‘gym’ yaliyoanza jana katika klabu ya Oil Com, iliyopo Chang’ombe, karibu na VETA jijini Dar es Salaam.

Meneja wa timu hiyo, Innocent Njovu, alizungumza na MTANZANIA na kusema kuwa wachezaji 11 wameanza mazoezi hayo na watano hawajafika, ukiacha walio katika timu ya taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’.

Njovu aliwataja wachezaji waliokacha mazoezi bila ya ruhusa kuwa ni Aziz Gilla na Shija Mkina, wakati wale walioomba ruhusa ni Mbwana Samata ambaye amefiwa na mama yake mlezi, Jerry Santo, yeye ameomba kuanza Jumatano na majeruhi Uhuru Seleman.

Meneja huo aliwataja wachezaji ambao wameanza mazoezi kuwa ni pamoja na Nahodha, Nico Nyagawa, Mussa Hassan ‘Mgosi’, Hillary Echessa, Amri Kiemba, Rashid Gumbo, Amir Maftah, Juma Jabu, Salum Kanoni, Kevin Chale na makipa wawili, Ali Mustapha ‘Barthez’ na Faraji Kabari.

“Mazoezi haya yataenda kwa wiki moja, halafu baada ya viungo vyao kurudi katika hali ya mazoezi wataanza mazoezi ya ufukweni, ili kuimarisha stamina ya miili yao kabla ya mazoezi ya kawaida ya kiufundi zaidi baada ya kocha kurudi,” alisema Njovu.

Alisema mazoezi hayo yanaendelea chini ya kocha msaidizi, Amri Said na kuwa wanatarajia kocha wao mkuu, Patrick Phiri kutua mara baada ya mashindano ya soka ya Afrika Mashariki na Kati, ‘Cecafa’ Chalenji kumalizika.

Njovu alisema wachezaji watapumzika siku chache kwa ajili ya sikukuu ya Krismasi na baada ya hapo watarudi na kuingia kambi ya kulala kwa ajili ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara, inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari 15, mwakani.
XxxxxMWISHO

No comments