ad

ad

KAOLE SNAKE PARK YATOA MSAADA WA MEZA NA VITI VYA WAALIMU WA SHULE YA MSINGI KAOLE.

Meneja wa kituo cha utalii wa ndani cha Kaole Snake Park Bagamoyo, David Kiguhe(kulia) akimkabidhi Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bagamoyo, Alex Mwakawago msaada wa Meza na Viti vya Waalimu wa Shule ya Msingi Kaole.Katikati ni Diwani wa Kata ya Dunda  Bagamoyo, Dickson Makamba na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kaole, Hamisi Juma Mrutu.Hafla fupi ya makabidhiano ilifanyika Kaole Snake Park Bagamoyo.

Meza 10 na Viti 10 zikiwa tayari kwa kukabidhiwa kama msaada kwa ajili ya Waalimu wa Shule ya Msingi Kaole Bagamoyo.


Na Mwandishi Wetu Bagamoyo.
KITUO cha Utalii wa ndani cha Kaole Snake Park kilichopo Bagamoyo Mkoa wa Pwani kimetoa msaada wa Meza na Viti vya Waalimu wa Shule ya Msingi Kaole vyenye thamani ya Shilingi milioni moja na laki nne katika hafla fupi iliyofanyika kituoni hapo mwishoni mwa wiki.
Akizungumza wakati wa makabidhiano Meneja wa Kaole Snake Park, David Kiguhe alisema kuwa msaada huo ni utekelezaji wa moja ya ahadi walizozitoa kwa Shule za ya Msingi Kaole wakati wa Hafla ya kuipongeza Shule kuwa namba moja katika ufaulu wa matokeo ya Mwaka jana.
Meneja David alisema kuwa waliahidi kuchangia kutoa msaada wa Meza 10 na Viti 10 vya Waalimu pamoja na kukarabati Vyoo vya Shule ya Msingi Kaole ambacho ndicho kitafuatia baada ya kutekeleza hili.
Kaole Snake Park iliteuliwa kuwa Mlezi wa Shule hiyo hivyo iko karibu na Shule na itaendelea kuwa karibu kama Mlezi kwa kutatua changamoto za Shule hiyo kwa kushirikiana na jamii inayoizunguka.
Nae Alex Mwakawago aliye mwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Elimu Bagamoyo, alishukuru sana Msaada huo uliotolewa na Kaole Snake Park na kuwapongeza Kaole Snake Park kukubali kuwa Walezi wa Shule ya Msingi Kaole.
Alisema Alex kwa niaba ya Mkurugenzi, msaada huu ni utekelezaji wa jamii kusapoti kauli ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuri ya Elimu bure.Jamii inapoona changamoto ndogondogo za Elimu na kuzitatua Serikali inatambua mchango wao katika sekta hii ya Elimu.
Tunaiomba Kaole Snake Park iendelee kuwa Mlezi wa Karibu kwa kusaidiana na jamii katika kuhakikisha maendeleo ya Shule ya Msingi yanaendelea kuwa mazuri na kwa jinsi hiyo basi alimtaka Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi kuhakikisha Shule ya Msingi Kaole iendelee kuwa namba moja kila mwaka.
Nae Diwani wa Kata ya Dunda, Dickson Makamba aliwashukuru sana Kaole Snake Park kwa msaada walioutoa na watakaoendelea kutoa na kutoa wito wasiishie Shule za Msingi Kaole wakiwa na nguvu zaidi waangalie na Shule zingine katika Kata yake ya Dunda, kwani changamoto za Elimu zipo nyingi sana.
Diwani Makamba alitoa wito pia kwa wawekezaji wengine wa hapa Bagamoyo kuiga mfano wa Kaole Snake Park kusaidia kupunguza Changamoto za Elimu pamoja na maendeleo ya Jamii kwa ujumla kwa kurudisha kidogo kwa Jamii inayowazunguka angalau mara moja kwa mwaka.
Nae Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kaole, Hamisi Juma Mrutu alishukuru sana msaada huo kutoka kwa Mlezi Kaole Snake Park na kuahidi kuendelea kushika namba moja kwa ufaulu kila mwaka kwani hana sababu ya kushindwa kama mahitaji yote anayoyahitaji yanapatikana.
Mwalimu Mkuu,Hamisi zaidi aliishukuru kamati ya Shule ndio iliyomuibua Mlezi huyo na kuwaomba kushirikiana nae kwa ukaribu sana kuitupia jicho la pekee Shule ya msingi Kaole.
Mwisho Kamati ya Shule ikiongozwa na Mwenyekiti, Mohamed Mbaruku ilishukuru sana msaada huo na kuahidi kushirikiana na Mlezi Kaole Snake Park kuhakikisha Shule ya Msingi Kaole inafanya vizuri daima.

No comments