KAMATI YA UTENDAJI TFF KUJADILI TAMKO LA SERIKALI

Baada ya kupokea barua hiyo jana alasiri (Februari 25
mwaka huu), Sekretarieti iliwasiliana na Rais wa TFF, Leodegar Tenga ambaye
ameagiza kuitishwa kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji kujadili tamko
hilo.
Kikao hicho cha Kamati ya Utendaji ya TFF kitafanyika
Jumamosi (Machi 2 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
KOCHA AZAM AFUNGIWA KWA KUCHOJOA BUKTA
KOCHA Mkuu wa Azam, Stewart John Hall amefungiwa mechi
tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 kwa kushusha bukta yake na kumlalamikia
mwamuzi msaidizi wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya timu yake
na Kagera Sugar iliyochezwa Januari 26 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex ulioko
Chamazi, Dar es Salaam.
Adhabu hiyo imetolewa na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana mwishoni mwa wiki kupitia ripoti za
michuano ya VPL na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2012/2013 inayoendelea
hivi sasa na kufanya uamuzi mbalimbali.
Naye Kocha Msaidizi wa timu ya Mgambo Shooting, Denis
Mwingira ametozwa faini ya sh. 500,000 kwa kumtolea lugha chafu mwamuzi kwenye
mechi dhidi ya Mtibwa Sugar iliyochezwa Oktoba mwaka jana katika Uwanja wa
Manungu.
Ally Jangalu ambaye ni Kocha Msaidizi wa Polisi Morogoro
naye ameangukiwa na rungu la Kamati ya Ligi kwa kupigwa faini ya sh. 500,000
baada ya kutolewa kwenye benchi kwa kupinga uamuzi wa refa kwa sauti ya juu.
Alitenda kosa hilo kwenye mechi kati yao na Kagera Sugar iliyochezwa Novemba 10
mwaka jana Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Matukio ya aina hiyo kwa kocha Jangalu yamekuwa ya
kujirudiarudia ambapo Oktoba 13 mwaka jana katika mechi dhidi ya Azam
iliyochezwa mjini Morogoro aliondolewa na mwamuzi kwenye benchi kwa kuchochea
wachezaji wa timu yake wacheze rafu.
Naye Kocha wa timu ya Moro United inayoshiriki FDL,
Yusuf Macho amepigwa faini ya sh. 200,000 kwa kumtolea lugha chafu refa baada ya
mechi dhidi ya Transit Camp iliyofanyika Novemba 4 mwaka jana Uwanja wa Mabatini
mjini Mlandizi.
Pia Kocha wa Burkina Faso, Hasheem Mkingie amepigwa
faini ya sh. 200,000 baada ya kutolewa kwenye benchi kwa kutoa lugha chafu
katika mechi ya FDL dhidi ya Mkamba Rangers.
Kiongozi wa Majimaji, Joseph Nswila ambaye aliingia
uwanjani baada ya mechi dhidi ya Mlale JKT kumalizika na kuvamia waamuzi
amefungiwa miezi sita.
Vilevile timu ya Azam imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa
kuchelewa kufika uwanjani kwenye mechi kati yao na JKT Oljoro iliyochezwa
Novemba 7 mwaka jana katika Uwanja wao wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es
Salaam.
Pia Coastal Union imetozwa faini ya sh. 500,000 kutokana
na washabiki wake kumrushia chupa za maji mwamuzi msaidizi namba mbili wakati wa
mechi yao dhidi ya Simba iliyochezwa Oktoba mwaka jana Uwanja wa Mkwakwani
jijini Tanga.
Nayo klabu ya African Lyon imepigwa faini ya sh. 500,000
kwa timu yake kugoma kuingia kwenye chumba cha kubadilishia nguo wakati wa
mapumziko katika mechi dhidi ya Coastal Union iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani
jijini Tanga, Oktoba 24 mwaka jana.
Timu ya Burkina Faso ya Morogoro imepigwa faini ya sh.
200,000 kutokana na kuonesha vitendo vya ushirikina kabla ya mechi yao dhidi ya
Mbeya City iliyochezwa Oktoba 24 mwaka jana Uwanja wa Jamhuri mjini
Morogoro.
Faini ya ushirikina ya sh. 200,000 pia imepigwa timu ya
Pamba baada ya kuonesha vitendo hivyo kwenye mechi yao dhidi ya Mwadui
iliyochezwa Novemba 4 mwaka jana Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Nayo Mkamba Rangers imepigwa faini ya sh. 200,000 baada
ya washabiki wake kumtolea lugha chafu Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa
wa Morogoro (MRFA), Hamis Semka na kumrushia chupa za maji mwamuzi wa mezani
katika mechi dhidi ya Mbeya City iliyochezwa mjini Morogoro.
Polisi Dodoma imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na
washabiki wake kuvamia uwanjani na kutaka kuwapiga waamuzi katika mechi yao
dhidi ya JKT Kanembwa na kusababisha mipira miwili ya Chama cha Mpira wa Miguu
Mkoa wa Dodoma (DOREFA) kupotea.
Pia klabu kadhaa zimeandikiwa barua za onyo kwa timu zao
kuchelewa kufika uwanjani au kutofika kwenye mkutano wa maandalizi ya mechi
(Pre-match meeting). Klabu hizo ni Coastal Union, JKT Ruvu, Toto Africans,
Simba, Green Warriors, Majimaji, Mkamba Rangers, Polisi Dodoma, JKT Kanembwa,
Moro United.
Mchezaji Stanley Nkomola wa JKT Ruvu baada ya mechi
dhidi ya Coastal Union alikwenda jukwaani na kuanza kupigana na washabiki. Pia
kipa wa timu ya Transit Camp, Baltazar Makene baada ya mechi dhidi ya Tessema
aliruka uzio na kwenda kupigana na washabiki.
Kwa vile masuala ya wachezaji hao ni ya kinidhamu
yamepelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu inayoongozwa na Kamishna wa Polisi (CP)
mstaafu Alfred Tibaigana kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.
MWAMUZI FIFA, MAHAGI WAONDOLEWA VPL
Mwamuzi Msaidizi wa FIFA, Ferdinand Chacha ameondolewa
kuchezesha mechi za VPL baada ya kupata alama za chini kwenye mechi kati ya
African Lyon na Simba iliyochezwa mwezi uliopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Waamuzi wanaopata alama 6.5 au chini ya hapo kati ya 10 zinazohitajika pia
wanaondolewa kwenye mechi za VPL na FDL.
Waamuzi wengine walioondolewa kwa kutomudu mechi
walizochezesha za VPL ni Mathew Akrama (Yanga vs Simba), Ephrony Ndissa (Yanga
vs Simba), Ronald Swai (Yanga vs Mtibwa Sugar).
Walioondolewa kwa kupata alama za chini ni Alex Mahagi
(Simba vs JKT Ruvu), Methusela Musebula (Toto Africans vs Coastal Union),
Lingstone Lwiza (Toto Africans vs Coastal Union), Idd Mikongoti (Toto Africans
vs Mtibwa Sugar) na Samson Kobe (Toto Africans vs Mtibwa Sugar).
Masoud Mkelemi aliyekuwa mwamuzi wa mezani katika mechi
ya FDL kati ya Moro United na Villa Squad ameondolewa kwa kutofika kwenye
mkutano wa maandalizi ya mechi (Pre-match meeting) na alichelewa kwa dakika tano
kufika uwanjani.
MAKAMISHNA VPL/FDL WASIMAMISHWA, WAONYWA
BAADHI ya makamishna wa VPL na FDL wameondolewa na
wengine kusimamishwa kusimamia mechi za ligi hizo kutokana na upungufu kwenye
ripoti zao au kutowasilisha kabisa ripoti hizo TFF baada ya mechi.
Kamishna Mohamed Jumbe aliyesimamia mechi kati ya Mgambo
Shooting na Simba ameondolewa kwenye orodha ya makamishna kutokana na ripoti
yake kuwa na upungufu.
Makamishna wa mechi kati ya JKT Oljoro vs Yanga (Hakim
Byemba), JKT Oljoro vs Kagera Sugar (Salum Kikwamba), Toto Africans vs African
Lyon (Charles Komba), Coastal Union vs JKT Oljoro (Mohamed Nyange)
wamesimamishwa hadi watakapowasilisha ripoti zao TFF.
Kwa upande wa FDL makamishna waliosimamishwa hadi
watakapowasilisha ripoti zao TFF ni wa mechi kati ya Kurugenzi vs Polisi Iringa,
Morani vs Mwadui, Polisi Mara vs Pamba, Polisi Mara vs Mwadui, Morani vs JKT
Kanembwa na Pamba vs Polisi Dodoma.
Wengine ni Mwadui vs JKT Kanembwa, Polisi Tabora vs
Morani, Polisi Dodoma vs Polisi Mara, Polisi Tabora vs Mwadui, Polisi Mara vs
Morani, JKT Kanembwa vs Polisi Mara, Morani vs Rhino Rangers na Small Kids vs
Mkamba Rangers.
Kamati ya Ligi imewakumbusha makamishna wote kuwa ni
jukumu lao kuhakikisha ripoti zao zimefika TFF na kurekebisha upungufu wa jinsi
ya kuripoti matukio yanayotokea uwanjani. Licha ya kutuma nakala kwa njia ya
email, wanatakiwa pia kuwasilisha ripoti halisi (original) TFF.
MECHI YA SIMBA, MTIBWA YAINGIZA MIL 62/-
MECHI namba 121 ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa juzi
(Februari 24 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa
Mtibwa Sugar kuibuka ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba imeingiza sh.
239,686,000.
Watazamaji 10,669 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo
ambayo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku
kila klabu ikipata mgawo wa sh. 14,577,252.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani
(VAT) iliyolipwa ni sh. 9,467,694.92.
Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji
wengi ambapo waliokata tiketi hizo walikuwa 9,491 na kuingiza sh. 47,455,000
wakati idadi ndogo ya washabiki ilikuwa ya kiingilio cha sh. 20,000 kilichovutia
washabiki 105 na kuingiza sh. 2,100,000.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja
sh. 7,412,162.26, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 4,447,297.36,
Kamati ya Ligi sh. 4,447,297.36, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh.
2,223,648.68 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh.
1,729,504.53.
VUMBI LA VPL KUENDELEA JUMATANO
MICHUANO ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa
Tanzania Bara inaendelea kesho (Februari 27 mwaka huu) kwa mechi
tano zitakazochezwa katika viwanja tofauti.
Vinara wa ligi hiyo Yanga wataikaribisha Kagera Sugar
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa viingilio vya sh. 5,000 (viti vya bluu
na kijani), sh. 8,000 (viti vya rangi ya chungwa), sh. 15,000 (VIP C na B) na
sh. 20,000 (VIP A).
Mechi nyingine za
ligi hiyo ni Coastal Union vs Ruvu Shooting (Mkwakwani, Tanga), Polisi Morogoro
vs Mgambo Shooting (Jamhuri, Morogoro), JKT Ruvu vs Toto Africans (Azam Complex,
Dar es Salaam) na Mtibwa Sugar vs Tanzania Prisons (Manungu,
Morogoro).
Post a Comment