CUF YAOMBA OPERESHENI YA KUWAKAMATA WAHALIFU IFANYIKE KITAALAMU
Mkurugenzi
wa Haki za Binadamu CUF Salim Bimani akifafanua jambo kupitia Katiba
katika mkutano wake wa kupinga matumizi mabaya ya Operesheni inayofanywa
na Jeshi la Polisi na Vikosi vya SMZ kuwatafuta wavunjifu wa
amani.Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar
……………………………………….
Chama cha Wananchi CUF
kimeliomba Jeshi la Polisi Zanzíbar kutumia mbinu za kitaalamu katika
kuwasaka na kuwakamata watu wanaodaiwa kuhusika na vitendo vya uvunjifu
wa amani katika ghasia zilizotokea karibuni ambazo pia zilisababisha
kuuliwa kwa Koplo wa Polisi Said Abdulrahman.
CUF kimelishauri Jeshi hilo
pamoja na Vikosi vya SMZ kuacha kuvamia makazi ya wananchi, na
kuwaadhibu kwa vipigo kwa madai ya kutekeleza Operesheni ya kuwatafuta
wahalifu wa matokeo hayo.
Akizungumza na Waandishi wa
Habari Ofisini kwake Vuga,Mkurugenzi wa Haki za Binadamu CUF Salim
Bimani amesema Operesheni ya kutumia uvamizi bila kutumia njia za
kitaalamu za kutafuta wahalifu zinakuza mgogoro uliopo badala ya
kuupunguza.
Amesema matendo ya uvunjifu
wa Amani na kuuliwa kwa Koplo Said Abdulrahman yanafanana na matukio ya
uvunjifu wa amani Tanzani Bara lakini Jeshi la Polisi Bara limekuwa
likitumia njia za kitaalamu katika kuwakamata wahalifu bila raia wengine
wasio na makosa kuathirika na Operesheni hiyo.
Ametoa mfano wa kuuliwa kwa
Kamanda wa Polisi Mwanza Liberatus Barlow na matukio ya uvunjifu wa
amani Dar es Salaam ambapo Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Vikosi
vya ulinzi viliweza kutuliza hali hiyo na kufanikiwa kuwakamata wahusika
na kupelekwa mahakani bila hata kuwaathiri wanachi ambao hawakuhusika
na kadhia hiyo.
Ameongeza kuwa Mahala popote
panapohitajika kufanywa Operesheni ya kuwasaka wahalifu mamlaka husika
ndizo zinazobeba dhamana na jukumu la kutumia uataalamu,mafunzo na mbinu
zinazoepusha ukiukwaji wa haki za binadamu na hatimaye kufanikisha
lengo.
Bimani
ameongeza kuwa CUF inalaani kwa nguvu zote vitendo vya fujo na uvunjifu
wa amani vilivyofanyika Octoba 17 hadi 19 vikijumuisha mauaji ya Koplo
Said, Salim Hassan Mahaju na Hamadi Ali Kaimu ambao wote waliuawa
kutokana na fujo hizo.
Kwa
upande wao baadhi ya wananchi ambao waliathirika na fujo hizo wameiomba
Serikali kuingilia kati operesheni hiyo na kutaka kutafutwe njia
stahiki za kuwakamata wahalifu bila ya kuwapiga au kuwanyanyasa ambao
hawahusika na fujo hizo.
Wamedai
kuwa tokea kuanzishwa kwa Operesheni hiyo wamekuwa hawana muda wa
kujishughulisha na kazi zao za kutafuta riziki badala yake wamekuwa
wakijifungia nyumbani mwao ili kujinusuru na vipigo.
Katika maeneo ambayo Operesheni hiyo imekuwa ikifanywa mara kwa mara ni Bububu, Amani, Magogoni, Daraja bovu, Mwanakwerekwe,Mtoni,Kinuni,Mboriborini,Mikunguni na Kwarara.
Post a Comment