ad

ad

JIJINI


Watatu watinga fainali kumsaka shujaa

Na Mwandishi Wetu, Ilala

WASHIRIKI watatu wameingia hatua ya fainali ya kumsaka shujaa wa Safari Lager ambaye atatafutwa Januari 21.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Meneja wa Safari Lager, Fimbo Butallah aliwataja washindi hao kuwa ni Mercy Shayo kutoka Kilimanjaro, Paul Luvinga na Leonard Mtepa wote wa Dar es Salaam.

“Tulipokea mapendekezo mengi toka kwa wananchi kuhusiana na mashujaa wao wakieleza mambo waliyofanya kwenye jamii na baada ya uchambuzi yakinifu, ndipo mashujaa hawa watatu wamefanikiwa kuingia fainali,” alisema Fimbo.

Alisema Mercy aliingia fainali baada ya kuisaidia jamii kwa kuwasaidia yatima kuhakikisha wanasoma akiwahudumia yeye, wakati Luvinga amefanikiwa kupata nafasi hiyo baada ya kujenga maktaba nyumbani kwake na kutoa huduma hiyo bure saa 24 na Mtepa yeye alimsaidia mjane kupata haki zake.

Tuzo ya shujaa wa safari Lager ilizinduliwa rasmi Novemba 24 mwaka jana ikiwa na lengo la kutambua na kuheshimu watu wanaofanya mambo makubwa yanayoleta mabadiliko kwa jamii inayowazunguka bila kusukumwa na uwezo wa pesa wala madaraka waliyonayo.

xxxxxMWISHO

Angetile, Wambura kuanika mikakati kesho

Na Mwandishi Wetu

KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah na Afisa Habari wake, Boniface Wambura jana walianza kazi rasmi katika shirikisho hilo na kuhaidi kuweka mikakati yao kesho.

Wakizungumza na waandishi wa habari, walisema kwa kuwa bado hawajakabidhiwa rasmi nyaraka na kuelekezwa mpango mzima wa shughuli, wanatarajia kukutana na waandishi wa habari kesho na kuweka hadharani namna utendaji kazi wao utakavyokuwa.

“Leo tumeingia rasmi ofisini, bahati mbaya hatujakabidhiwa mafaili kwa kuwa Sunday Kayuni aliyekuwa akikaimu ameondoka na timu yetu ya Taifa ‘Taifa Stars’ iliyokwenda Misri kushiriki michuano ya Nile Basin,” alisema Angetile.

Alisema kwa kuwa ipo siku ya leo, wana imani watapata fursa ya kupewa maelekezo na hivyo kesho (Jumatano) itakuwa ni nafasi nzuri kwao kuzungumza na waandishi namna watakavyoliongoza Shirikisho hilo.

Angetile alisema mkutano kati yao na wana habari utakuwa ni kuzungumza kwa kina namna gani pande hizo zitakuwa zikifanya shughuli zake za kila siku pamoja na kutambulishana rasmi.

xxxxxMWISHO

BMT yatoa mafunzo ya michezo Iringa

Na Jennifer Ullembo, Temeke

BARAZA la michezo nchini (BMT), jana lilianza kutoa mafunzo ya michezo mkoani Iringa .

Akizungumza na Mtanzania Mratibu wa mafunzo hayo Mohamed Kiganja alisema wameamua kuendesha mafunzo hayo kwa walimu 15 wa sekondari na 10 wa shule ya msingi ili kuwajengea uwezo katika fani hiyo.

“Tunatoa mafunzo haya kwani hawa ndiyo watakao weza kukuza michezo shuleni hivyo ni vizuri wakipata mafunzo kiundani zaidi,”alisema Kiganja.

Mafunzo hayo yanafadhiliwa na BMT kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mufindi yanatarajiwa kumalizika Januari saba.

xxxxxxMWISHO.

Mapacha watatu kupagawisha Coco Beach

Na Mwandishi Wetu,Kinondoni

BENDI ya muziki wa dansi ya Mapacha Watatu, leo itatoa burudani katika ufukwe wa Coco Beach.

Akizungumza na Mtanzania, mmoja wa wakurugenzi wa bendi hiyo, Jose Mara, alisema onyesho hilo ni sehemu ya kuonyesha ubora wao.

Alisema mashabiki wao waje kwa wingi katika kujionea moto wa Mapacha Watatu, bendi iliyoasisiwa kwa mbwembwe mwishoni mwa mwaka jana.

“Kila Jumanne, siku kama ya kesho (leo) hufanya shoo katika ukumbi wa kando kando ya baa inayopatikana katika ukumbi huo wa Coco Beach.

“Nadhani mikakati yetu ni kuhakikisha kwamba bendi yetu inakuwa kwenye mafanikio makubwa katika kona ya muziki wa dansi hapa nchini,” alisema.

Bendi hiyo yenye mashabiki wengi nchini, inafanya mambo mazito ya kuhakikisha kwamba wanaonyesha ubora wao.


No comments