ad

ad

Mzambia Yanga atoa somo

Mzambia Yanga atoa somo

Na Deborah Kajolo

MSHAMBULIAJI mpya wa Yanga, Davies Musonda Mwape, amewataka wachezaji wenzake kumpa ushirikiano ili kufanikisha malengo ya klabu hiyo.

Akizungumza na Mtanzania juzi, alisema kwa sasa anaweza kuzungumza lolote na vyombo vya habari kwani ni mchezaji halali wa Yanga na kikubwa anachoomba kwa wachezaji wenzake hata akiwa kambini ni ushirikiano.

Alisema Yanga ipo katika nafasi nzuri katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, hivyo uwezekano wa kujipanga na kuchukua ubingwa huo upo lakini hilo litategemea ushirikiano wao wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki.

“Nitajitahidi kuitumikia Yanga kwa uwezo wangu wote ili kutimiza lengo lililomleta hapa nchini na nipo tayari kupokea ushauri wowote kutoka kwa wenzangu, viongozi na hata mashabiki,” alisema Mwape.

Alisema atautumia vema muda wa maandalizi ya kuelekea mzunguko pili wa ligi kuzoeana na wachezaji wenzake, kwani hiyo itawasaidia kucheza vizuri duru hilo la lala salama.

Yanga inashika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 25 katika Ligi Kuu Bara na imeongeza wachezaji wawili katika usajili wa dirisha dogo kwa kumsajili Mwape na Salum Seif wa JKT Ruvu ya Pwani.

xxxxxMWISHO


Taifa Queens yaenda Singapore

Na Jennifer Ulembo

WACHEZAJI 12 wanaounda timu ya Taifa ya Netiboli, ‘Taifa Queens’ wamekwenda Singapore kwa ajili ya kushiriki mashindano ya kusaka viwango.

Mashindano hayo yamepangwa kuanza kesho hadi Desemba 12 na yameandaliwa na Shirikisho la Kimataifa la Netiboli (IFNA).

Akizungumza na Mtanzania, nahodha wa timu hiyo Jackline Sikozi, alisema wanakwenda huko kuhakikisha wanafanya vema katika michuano hiyo ili kuliletea sifa Taifa.

“Tumefanya mazoezi ya kutosha tunaimani tutarudi na ushindi tuombeeni Mungu tufike salama na kurudi,”alisema Sikozi

Katika mashindano hayo, jumla ya nchi sita ikiwamo Tanzania, zinatarajiwa kushiriki huku Tanzania ikiwakilishwa na wachezaji 12 na viongozi wanne.

Wachezaji hao ni Lilian Sylidion, Irene Elias, Lidya Samweli, Restituta Boniphace, Eva Peter, Veronica Kuburi, Sekela Dominick, Mwanaidi Hassan, Paskalia Kibayasa, Zuhura Twalibu.

Viongozi ni Kocha mkuu wa timu hiyo Simone Mckinns, msaidizi wake Damian Choya na daktari Richard Yomba.
xxxxxxxxMWISHO

Swahili Fashion yaandaa siku ya Ukimwi

Na Mohamed Mharizo

WAANDAAJI wa Tamasha la mavazi nchini, ‘Swahili Fashion Week’ wameandaa sherehe ya Siku ya Ukimwi itakayofanyika leo katika Ukumbi wa Mercury visiwani Zanzibar.

Tukio hilo limeandaliwa kwa ushirikiano na Kampuni ya Explore Zanzibar kwa lengo la kutunisha Mfuko wa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi (ZAPH).

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mratibu wa Swahili Fashion Mustapha Hassanali alisema ni jukumu la jumuiya na kila mmoja kuwasaidia watu wanaoishi na virusi vya ukimwi.

“Ni jukumu letu na kwa kila mmoja wetu na jumuiya kwa ujumla kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii, tukijua kwamba Swahili Fashion Week imelenga katika kuwasaidia watu waishio na virusi vya ukimwi,”alisema.

Wakati huo huo, mbunifu wa mavazi nchini, Manju Msita amechaguliwa kuiwakilisha Tanzania katika tamasha la Mozambique Fashion litakalofanyika kuanzia Desemba 6 hadi 11 jijini Maputo, Msumbiji.

xxxxxxxxMWISHO
Toto African yahofia mzunguko wa pili


Na Jennifer Ullembo

KOCHA Mkuu wa timu ya Toto African, Choke Abed amekiri mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania utakaoanza Januari 15 utakuwa mgumu.

Akizungumza na Mtanzania, Choke alisema zinahitajika juhudi kubwa hasa upande wa wachezaji wanapaswa kupewa mazoezi ya kutosha.

“Mzunguko wa pili utakuwa mgumu ukizingatia timu nyingi zimesajili wachezaji wazuri dirisha dogo,” alisema.

Alisema timu yake imejiandaa vizuri na hatokubali kufungwa. Timu hiyo imepanga kuanza mazoezi Desemba 15.


“Tukiwa kambini tutajitahidi, pia tuna mpango wa kucheza mechi mbili za kirafiki Musoma na Ukerewe,” alisema.
XXXXXMWISHO


Ma ‘Pro’ wa Yanga wawasili

Na Kambi Mbwana

WACHEZAJI watatu wa Kimataifa wa klabu ya Yanga, Isaac Boakye, Enock Boakye na Yew Berko wamewasili jana tayari kuanza mazoezi na timu hiyo yaliyopangwa kuanza leo Uwanja wa Shule ya Kimataifa ya Tanganyika.


Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Ofisa habari wa Yanga, Louis Sendeu, alisema kuwasili kwa wachezaji hao ni sehemu ya maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom iliyopangwa kuanza Januari 15.

“Tunataka kufanya maandalizi kabambe chini ya kocha wetu, Kostadin Papic, naamini kila kitu kitakwenda sawa,” alisema Sendeu.
xxxxxxxMWISHO

No comments