ad

ad

Mama Salma Kikwete awataka wanafunzi wa kike kujiepusha na Mafataki


Na Anna Nkinda – Maelezo

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amewataka wanafunzi wa kike kujiepusha na mafataki ambao watawarubuni kwa vitu mbalimbali na hatimaye kuwapatia ujauzito na ugonjwa wa Ukimwi na hivyo kutofikia malengo waliyojiwekea katika maisha yao.

Pia amewataka wanafunzi  wa kiume kuachana na tabia ya kuvaa suruali milegezo na uvutaji wa sigara ambao utawasababishia kupata ugonjwa wa kansa ya koo na mapafu.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ameutoa wito huo hivi karibuni wakati akiongea na wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Msimbu iliyopo kata ya Msimbu wilaya ya Kisarawe  mkoani Pwani.

“Kama wazazi wenu hawawasimanii kufuatilia  mienendo yenu mjisimamie nyinyi wenyewe kwa kukanyana na kutoa taarifa kwa walimu wenu pale ambapo mtaona mwenzenu ana tabia ambazo ni kinyume na maadili ya mwanafunzi  kwa kufanya hivyo mtaepukana na tatizo la mimba za utotoni’, alisema Mama Kikwete.

Kuhusiana na madai ya wanafunzi hao kuwa wazazi wao wanakabiliwa na tatizo la umaskini jambo ambalo linawafanya waweze kuingia katika vishawisi mbalimbali Mama Kikwete alisema kuwa umaskini isiwe ni kigezo cha mtu kufanya mambo yasiyofaa ili aweze kupata fedha jambo ambalo ni  hatari katika maisha yake.

“Ni muhimu wazazi wakatafuta mbinu mbadala ya kuweza kukabiliana na hali hii ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwani mtu akifanya kazi kwa bidii ni lazima atafanikiwa na kuweza kupambana na hali ya umaskini kwani atalima mazao na kuuza, atafanya biashara ndogondogo na kuweza kujipatia kipato”, alisema Mama Kikwete.

Aidha Mama Kikwete pia aliwataka wanafunzi hao kuitumia teknolojia vizuri katika kujiletea maendeleo ikiwa ni pamoja na kujitafutia nyaraka za kusoma “material” kwa ajili ya masomo yao na siyo tofauti kwani teknolojia ikitumika vibaya ni rahisi mtu kuiga mambo ambayo  ni tofauti na utamaduni wake.

Akisoma taarifa ya shule hiyo Mwalimu Mkuu Renatus Rweyemamu alisema kuwa tangu shule hiyo ilipoanzishwa mwaka 2007 hadi sasa idadi ya wasichana waliopata ujauzito ni 34 na wahusika wameshafikishwa kwenye vyombo vya dola na hivi sasa suala hilo linasimamiwa na watendaji wa vijiji husika.

Alizitaja changamoto zinazoikabili shule hiyo kuwa ni wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata shule jambo ambalo linasababisha kuingia darasani wakiwa wamechoka pia wasichana wanakutana na vishawishi vingi wakiwa njiani, hosteli moja haitoshi kwa kuwa  inauwezo wa kuchukua wanafunzi 48 pia haina vitanda wala magodoro ya kulalia.

Mwalimu  Rweyemamu alisema, “Changamoto nyingine ni wazazi kutofuatilia kwa ukaribu mienendo ya watoto wao pia kutokutoa ushirikiano wakati wa  kuwafuatilia wahusika waliowapatia  ujauzito watoto wao”.

Aliiitaja mikakati waliyojiwekea kuwa ni kufanya mikutano na wazazi ili kuwapa ushauri jinsi gani wanaweza kufuatilia mienendo ya watoto wao na kutafuta wafadhili watakaowasaidia kujenga Hosteli ikiwa ni pamoja na kununua vitanda, magodoro na kuweka umeme jua.

“Pamoja na majukumu mengi yanayokukabili ombi letu kubwa kwako kwa sasa ni tunaomba kama itawezekana utununulie vitanda na magodoro kwa Hosteli yetu”, alisema Rweyemamu.

Shule ya Sekondari ya Msimbu ni shule ya kata ambayo inajumla ya wanafunzi 463 wasichana wakiwa ni 250 na wavulana 213 ambao wanatoka katika vijiji sita vilivyopo katika kata ya Msimbu.

No comments